Shaa katika pozi |
MCHAKATO wa kusaka madansa watakapamba jukwaa la msanii Sarah Kais 'Shaa' umeanza ukiendeshwa na mabosi wa msanii huyo, kituo cha Mkubwa na Wanae.
Mkurugenzi wa kituo hicho na meneja wa Shaa, Said Fella alisema tayari wameanza kupokea wasanii wanaotaka kuwa miongoni mwa madansa hao wanne kabla ya kuanza kuwafanyia usaili kisha wale watakaokithi viwango kushindanishwa kusaka madansa wanne wa kuunda kundi la Shaa.
Fella alisema mchakato wa kuwashindanisha madansa huo utafanyika kwa utaratibu maalum katika kundi zitakazotangazwa ndani ya wilaya ya Temeke kabla ya fainali ya mwisho kufanyika katika ukumbi mmoja maarufu hapa jijini Dar.
'Tumeshaanza kupokea madansa wanaotaka kuwania kuwa miongoni mwa madansa wanne wa Shaa, tutawachuja kisha wale watakapita watashindanishwa ili kusaka wanne wa mwisho watakaoambatana na Shaa katika maonyesho yake," alisema.
Aidha Fella alisema wimbo mpya na wa pili wa Shaa uitwao 'Sifa Ujinga' umeshakamilishwa na sasa unaandaliwa video yake ndipo vtyote viachiwe hadharani.
Pia alisema wameona isingekuwa vyema kuutoa wimbo huo mpya wakati wimbo wa 'Sugua Gaga' ulioachiwa hivi karibuni ukiendelea kutesa katika vituo vya redio na runinga.