STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, February 25, 2013

TIMBULO KAKAMATWA BURUNDI NA MADAWA YA KULEVYA?


Kuna tetesi kuwa msanii wa Bongo flava maarufu kwa jina la Timbulo, ambaye amepata umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wa kuimba katika nyimbo zake kadhaa kama  Domo Langu, Waleo Wakesho, Samson na Delilah, amekamatwa mjini Bujumbura kwa tuhuma za kukutwa na madawa ya kulevya. Timbulo alikuwa huko katika kufanya mipango ya kufanya maonyesho kadhaa nchini Burundi mwezi April mwaka huu.
CHANZO:SANAA NA WASANII TANZANIA

BREAKING NEWS: WAZIRI WA MICHEZO AFUTA KATIBA YA TFF, KISA

 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk Funella Mukangara
SERIKALI imeingilia kati sakata la uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuamuru kufutwa kwa katiba ya sasa ya shirikisho hilo na badala yake kuamuru itumike katiba ya zamani (mwaka 2006) baada ya kubaini kuwa iliyopo ina kasoro nyingi.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari leo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo imeeleza kuwa katiba ya sasa ya TFF si halali. Imeelezwa vilevile kuwa msajili wa vyama vya michezo aliyedaiwa kuipitisha katiba hiyo ameondolewa.

Mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF umesimamishwa kutokana na mgogoro mzito uliotokana na kuenguliwa kiutata kwa wagombea kadhaa, wakiwamo Jamal Malinzi anayewania urais na Michael Wambura anayetaka kugombea nafasi ya makamu wa rais.

Kamati ya rufani ya TFF inayoongozwa na Iddi Mtiginjola ndiyo iliyozua balaa lote la sasa baada ya kuwaengua kina Malinzi na mwishowe kumuacha makamu wa sasa wa rais, Athumani Nyamlani abaki kuwa mgombea pekee.


Hata hivyo, tayari mchakato wa uchaguzi huo uliozua mabishano makali umeshasimamishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na maafisa wa chombo hicho cha juu cha mchezo wa soka duniani wameshaanza kuwasili kufuatilia kinachotokea nchini.

Uamuzi wa serikali wa kufuta katiba ya sasa na kutaka itumike ya 2006 unampa ahueni kubwa Wambura ambaye alishasema hadharani kuwa  ataiburuza TFF mahakamani kama isipoachana na katiba mpya na kufuata ya zamani; huku akitoa sababu kadhaa za kupinga matumizi ya katiba mpya, mojawapo ikiwa ni kupitishwa kwake kwa njia ya waraka wa barua pepe (e-mail) kwenda kwa wajumbe badala ya kufuata maelekezo ya katiba yanayotaka mabadiliko kufanywa na wajumbe kupitia mkutano mkuu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu za FIFA, ni marufuku kwa shughuli za soka kuingiliwa na serikali au mahakama na nchi yoyote inayokwenda kinyume na taratibu hizo hujikuta ikifungiwa kama ilivyowahi kutokea enzi za FAT au ilivyoikumba nchi ya Kenya.

PAMBANO LA GOLDEN BUSH VETERANI VS CLOUDS KATIKA PICHA


Kikosi cha Clouds The Dream Team

Wachezaji wa timu za Golden Bush na Clouds wakiwa katika picha ya pamoja

Kikosi cha Golden Bush kilichoipa kichapo cha mabao 4-1 Clouds The Dream Team

Kivumbi uwanjani

Shija Katina (8) Nahodha wa Golden Bush katika harakati zake uwanjani na vijana wa Clouds

Mchezaji wa Clouds akitafuta wapi pa kupeleka pasi kwa wenzake

Shija Katina na wachezaji wa Cl;ouds wakiusaka mpira


Said Swedi 'Panucci' aliyefunga mabao mawili kati ya manne ya Golden Bush akiambaa na mpita, huku akinyemelewa na Shafii Dauda (kulia)

Baadhi ya mashabiki wa Clouds wakiwa hawaamini kama wamelala kwa Golden Bush

Mkali Shafii Dauda


Shafii Dauda akionyesha kiwango chake katika soka, sio kutangaza tu!

MAN II MAN: Majaliwa (14) beki wa Golden Bush akimchunga Ben KInyaiya, mfungaji wa bao la kufutia machozi la Clouds katika mechi iliyochezwa juzi jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE ZIMEHAMISHWA SHAFII DAUDA)

YANGA, AZAM KITANZINI, KISA VURUGU

Polisi wakidhibiti vurugu zilizotokea mara baada ya pambano la Yanga na Azam juzi

KLABU ya Yanga inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Azam inayoifuata huenda zikakumbana na adhabu kali kufuatia makosa mbalimbali yakiwamo ya vitendo vya vurugu vilivyojitokeza katika mechi yao ya ligi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 lililowekwa wavuni na kiungo wake wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima 'Fabregas' ambapo baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, vurugu zilizidi na watu kadhaa walijeruhiwa.
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Kamati ya Ligi itakutana mara tu baada ya kupokea ripoti ya waamuzi na kamishna wa mechi mechi hiyo kabla ya kutoa maelekezo juu ya nini kitakachofuata.
Akieleza zaidi, Wambura alisema kuwa watu kibao waliokuwapo uwanjani walishuhudia kila kilichotokea, baadhi yao wakiwa ni maafisa wa TFF (akiwamo yeye) na kwamba, kinachosubiriwa ni ripoti rasmi tu kutoka kwa waamuzi na kamishna ambao hawapaswi kuingiliwa majukumu yao.
"Ripoti ikishakuwa tayari na kuonekana kuwa kuna makosa,  yale ya kinidhamu yatapelekwa kwenye kamati ya nidhamu," alisema Wambura.
Miongoni mwa matukio yaliyoonekana juzi baada ya kumalizika kwa mechi, ni baadhi ya mashabiki waliodhaniwa kuwa wa Azam kutaka kumvamia refa aliyechezesha mechi hiyo na hata baada ya polisi kuingilia kwa nia ya kumlinda (refa), baadhi ya mashabiki hao wakataka kutwangana na askari pia. Watu hao walikuwa wakimtuhumu refa kuwa ameipendelea Yanga, hasa kwa kukataa goli lililofungwa na John Bocco katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza kwavile halikuwa halali.
Katika mechi mojawapo ya msimu uliopita baina ya timu hizo, kuliibuka vurugu pia ambapo refa alidaiwa kuibeba Yanga wakati 'wanajangwani' wakipata kipigo kikali cha mabao 3-1. Yanga walioonekana wazi wakitaka kumpiga refa Israel Nkongo walikumbana na adhabu kali ikiwa ni pamoja na kulimwa faini kwa wachezaji wake kadhaa na baadhi yao kufungiwa kwa vipindi tofauti.


CHANZO:NIPASHE

SIMBA HATARINI KUPOROMOSHWA ZAIDI

Kikosi cha Coastal Union

WAKATI wakijiandaa na safari yao ya Angola kwa ajili ya pambano la marudiano la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Libolo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ipo hatarini kuporomoka zaidi kwenye msimamo wa ligi iwapo Coastal Union itashinda pambano lake dhidi ya Ruvu Shooting keshokutwa.
Coastal inatarajiwa kuvaana na Shooting Jumatano kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga, ambapo ushindi wowote itakaopata utaifanya ifikishe poiinti 33 na hivyo kuiengua Simba yenye piointi 31 ambayo haitakuwa dimbani nchini katika ligi hiyo.
Japo Coastal iliyorekebisha makosa kwa kuinyuka Oljoro katika mechi yake iliyopita, isitarajie mteremko kwa Ruvu kwani maafande hao katika mechi zao za duru la pili wameonekana kuimarika zaidi, hivyo huenda ikapata upinzani mkali iwapo watataka kukalia nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hiyo.
Mechi nyingine zitakazochezwa siku hiyo ni pamoja na pambano la kukata na mundu kati ya Yanga na Kagera Sugar ambayo jana ililazimishwa sare ya bao 1-1 na wageni wao African Lyon katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Kaitaba.
Katika mechi yao ya awali Yanga ilicharazwa bao 1-0 na Kagera na kuibua hisia kali kwamba kuna baadhi ya wanahabari walitumika kuihujumu timu na kupelekea kutolewa vitisho na kuwapiga marufuku waandishi hao walioambatana na timu hiyo toka Dar kukaa mbali na kambi yao.
Yanga itahitaji ushindi ili kuimarisha nafasi yake ya kukaa kileleni kutokana na kwamba timu inazowafukuza kwa karibu Azam na Simba watakuwa kwenye mechi za kimataifa ugenini mwishoni mwa wiki.
Iwapo Yanga itashinda itafikisha pointi 41 ikiwa michezo sawa na Azam wenye pointi 36 na kuiacha Simba kwa pointi 10 kitu kitakachoiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Michezo mingine kwa siku ya Jumatano kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo ni Polisi Moro itakayoikaribisha Mgambo JKT uwanja wa Jamhuri Morogoro, JKT RUvu dhidi ya Toto African mechi itakayochezwa uwanja wa Chamazi na 'wababe wa Simba' Mtibwa Sugar watakuwa viwanja vyao vya Manungu Complex kuikaribisha Prisons ya Mbeya.

Msimami kamili wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya mechi za mwishoni mwa wiki ni kama ifuatavyo:



          P W D L GF GA GD Pts
1 Young Africans FC Young Africans 17  12  3 2 33 12 21 39
2 Azam FC Azam 18  11 3 4 31 15 16 36
3 Simba SC Simba 18 8 7 3 26 15 11 31
4 Coastal Union  18 8 6 4 21 16 5 30
5 Kagera Sugar FC Kagera Sugar 18 7 7 4 19 16 3 28
6 Mtibwa Sugar FC Mtibwa Sugar 18 7 6 5 21 18 3 27
7 Ruvu Shooting Stars Ruvu Shooting  16 7 4 5 20 17 3 25
8 JKT Mgambo 17 6 3 8 13 16 -3 21
9 JKT Oljoro 18 5 6 7 19 22 -3 21
10 Prisons-Mbeya 16 4 6 6 10 13 -3 18
11 JKT Ruvu Stars JKT Ruvu Stars 16 4 4 8 14 26 -12 16
12 Toto African Toto African 19 2 8 9 15 28 -13 14
13 African Lyon FC African Lyon 19 3 4 12 13 31 -18 13
14 Polisi Moro 16 2 5 9 8 18 -10 11


FIFA KUCHUNGUZA KWA KINA MCHAKATO WA UCHAGUZI TFF


OFISA Maendeleo wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi amewahakikishia Watanzania kuwa ujumbe wa Shirikisho hilo utakaokuja nchini mwezi ujao, utafanya uchunguzi wa kina kuhusu mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (FIFA) na kutoa uamuzi kwa maslahi ya mchezo huo.

“Ninafurahi kwamba hali ya utulivu imefikia kiwango hiki na nina uhakika FIFA itafanya uchunguzi wa kina na kufanya uamuzi kwa maslahi ya mpira wa miguu,” amesema Mamelodi alipokuwa akizungumzia uchaguzi mkuu wa TFF ambao ulikuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu lakini ukasimamishwa kutokana na matatizo kadhaa baada ya baadhi ya wagombea kuenguliwa.

Mbali na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa TFF na uchaguzi, safari ya Mamelodi nchini pia ilihusisha kumtambulisha msaidizi wake, Patrick Onyango ambaye amejiunga na ofisi hiyo ya FIFA kuanzia mwishoni mwa mwaka jana, kufuatilia miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na GOAL Project 4 ambayo ni uwekaji wa nyasi bandia kwenye Uwanja wa Nyamagana na maendeleo ya Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, mikakati ya mwaka 2013 na kozi mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Mikutano wa TFF jana, Mamelodi alisema uamuzi wa Shirikisho hilo kutuma wajumbe katikati ya mwezi ujao unatokana na mawasiliano baina ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga na FIFA ambayo ilitaarifiwa hali halisi ilivyo na kama inaweza kusaidia kutatua matatizo yaliyopo.

“FIFA haitakuja kuingilia mchakato wa uchaguzi, itakuja kutatua matatizo,” amesema Mamelodi. “Masuala ya uchaguzi ni ya ndani ya nchi. FIFA haiji kuichagulia Tanzania rais. Wajumbe wanaweza kumchagua mtu yeyote wanayeona kuwa anafaa kuwa rais,” amesema Mamelodi.

“Lakini katiba ya FIFA iko wazi kwamba mwanachama wake ni lazima akubaliane na sheria za Shirikisho kuwa wanachama ni lazima wabanwe na Katiba ya FIFA. Kwa hiyo mara tu unapopata uanachama wa FIFA, ni lazima ujue kuwa utabanwa na katiba ya FIFA na mojawapo ya mambo haya.

“Lakini kuna tofauti na kitendo cha Serikali kusimamisha uchaguzi kwa kuwa hiyo inakuwa ni Serikali kuingilia moja kwa moja masuala ya mpira wa miguu, kitu ambacho katiba ya FIFA inakataza.”

Mamelodi, ambaye alitumia muda mwingi kuelezea umuhimu wa hali ya utulivu iliyotawala kwa muda mrefu nchini, amesema anajua kuwa uongozi wa Rais wa sasa wa TFF, Leodegar Tenga umefanya mengi katika kuhakikisha unajenga mazingira mazuri ya maendeleo ya mpira wa miguu, lakini kuna wakati ni lazima uheshimu uamuzi wa mtu.

“Tenga amesema imetosha anaondoka na hatuna budi kuheshimu uamuzi wake. Hiyo ni kauli inayotoka kwa kiongozi wa kweli, kiongozi anayewajibika. Lakini kwa kuangalia misingi ambayo uongozi wake umeijenga, ni wazi kuwa kiongozi mpya ataendeleza taasisi bila ya matatizo.

“Tanzania haikufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, lakini kuna miradi mingi ya maendeleo ambayo ilifanyika, mingine ambayo ilijaribiwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania na ikafanikiwa. Kuna Azimio la Bagamoyo, Semina ya Mawasiliano ya Jamii (Comm-Unity) ya Wanawake, Futuro III na mingine. Yote hii ilifanyika kwa sababu kulikuwa na utulivu.

“Hivi sasa TFF ina sekretarieti ina Mkurugenzi wa Ufundi; ina programu za maendeleo na kuna utulivu. Cha msingi ni kuendeleza haya. Kama mambo haya yataendelezwa baada ya uchaguzi, ni dhahiri kuwa mpira utazidi kuendelea. Hakuna njia ya mkato katika maendeleo.”

Uchaguzi wa TFF ulihusisha nafasi za rais, makamu wa rais na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka Kanda 13 za Shirikisho.

Angetile Osiah
Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)