STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, February 25, 2013

YANGA, AZAM KITANZINI, KISA VURUGU

Polisi wakidhibiti vurugu zilizotokea mara baada ya pambano la Yanga na Azam juzi

KLABU ya Yanga inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Azam inayoifuata huenda zikakumbana na adhabu kali kufuatia makosa mbalimbali yakiwamo ya vitendo vya vurugu vilivyojitokeza katika mechi yao ya ligi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 lililowekwa wavuni na kiungo wake wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima 'Fabregas' ambapo baada ya filimbi ya mwisho kupulizwa, vurugu zilizidi na watu kadhaa walijeruhiwa.
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Kamati ya Ligi itakutana mara tu baada ya kupokea ripoti ya waamuzi na kamishna wa mechi mechi hiyo kabla ya kutoa maelekezo juu ya nini kitakachofuata.
Akieleza zaidi, Wambura alisema kuwa watu kibao waliokuwapo uwanjani walishuhudia kila kilichotokea, baadhi yao wakiwa ni maafisa wa TFF (akiwamo yeye) na kwamba, kinachosubiriwa ni ripoti rasmi tu kutoka kwa waamuzi na kamishna ambao hawapaswi kuingiliwa majukumu yao.
"Ripoti ikishakuwa tayari na kuonekana kuwa kuna makosa,  yale ya kinidhamu yatapelekwa kwenye kamati ya nidhamu," alisema Wambura.
Miongoni mwa matukio yaliyoonekana juzi baada ya kumalizika kwa mechi, ni baadhi ya mashabiki waliodhaniwa kuwa wa Azam kutaka kumvamia refa aliyechezesha mechi hiyo na hata baada ya polisi kuingilia kwa nia ya kumlinda (refa), baadhi ya mashabiki hao wakataka kutwangana na askari pia. Watu hao walikuwa wakimtuhumu refa kuwa ameipendelea Yanga, hasa kwa kukataa goli lililofungwa na John Bocco katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza kwavile halikuwa halali.
Katika mechi mojawapo ya msimu uliopita baina ya timu hizo, kuliibuka vurugu pia ambapo refa alidaiwa kuibeba Yanga wakati 'wanajangwani' wakipata kipigo kikali cha mabao 3-1. Yanga walioonekana wazi wakitaka kumpiga refa Israel Nkongo walikumbana na adhabu kali ikiwa ni pamoja na kulimwa faini kwa wachezaji wake kadhaa na baadhi yao kufungiwa kwa vipindi tofauti.


CHANZO:NIPASHE

No comments:

Post a Comment