CHAMA cha
Wananchi (CUF) kimesema hakiikubali Katiba inayopendekezwa kwa kuwa
haina maslahi ya wananchi wa Zanzibar.
Badala yake chama hicho kimewataka
Wazanzibari waikatae Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba
(BMK).
Kauli
hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, wakati akihutubia
mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Demokrasia vya Kibanda
Maiti, mjini Zanzibar.
“Wananchi,
Katiba haikubaliki kwa Wazanzibari, mimi mwenzenu siikubali, sijui
nyinyi wenzangu?” alihoji Maalim Seif na wananchi kuitikia kuwa nao
hawaikubali.
Alisema
kuwa miongoni mwa mambo yanayoipokonya Zanzibar hadhi yake ni Katiba
inayopendekezwa kumpokonya Rais wa Zanzibar mamlaka ya kugawa mikoa,
tofauti na Katiba ya Zanzibar ya sasa.
Alisema
kwa maana hiyo Rais wa Muungano anachukua mamlaka ya Rais wa Zanzibar
na anaweza kuteuliwa wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya wa Zanzibar.
“Kwa
mabadiliko hayo ya rasimu ya Chenge, Rais wa Muungano anaweza
kututeulia Sheha wa Shehia ya Mtoni Zanzibar kutoka Bukoba,” alisema
Maalim Seif huku akishangiliwa na wanachama na wafuasi wa CUF.
Maalim
Seif alisema Katiba ya Zanzibar na marekebisho yake ya mwaka 2010 iko
sahihi kabisa na inazingatia matakwa ya Makubaliano ya Muungano.
Alisema hayuko tayari kuona rasimu hiyo inakubalika na kwamba Wazanzibari hawataki kuiona.
Alisema
hakubaliani na kauli za baadhi ya watu waliosema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inaridhishwa na mchakato wa Katiba mpya.
“Nataka
kuwambia hakuna kikao chochote cha SMZ kilichokaa na kusema tunaijadili
rasimu, kama kuna mtu anataka kusema eti Smz imeridhishwa aseme
mwenyewe binafsi na siyo Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Maalim
Seif.
Maalim
Seif aliisifu Rasimu ya Jaji Joseph Warioba ambayo ndiyo ilizingatia
matakwa ya Watanzania walio wengi na kwamba pamoja na awali Wazanzibari
kupendekeza muundo wa Muungano wa mkataba, lakini kwa busara ya tume
hiyo waliikubali muundo wa serikali tatu.
Maalim
Seif alisema anahutubia mkutano huo akiwa na furaha kubwa kutokana na
umma ulioteremka katika viwanja vya Kibandamaiti, na hiyo ni sababu
tosha na ujumbe kuwa hawaitaki Katiba inayopendekezwa.
“Ndugu
yangu, rafiki yangu Rais Jakaya Kikwete ufahamu kuwa umma huu
uliohudhuria Kibandamaiti ni ujumbe tosha kuwa Katiba hiyo hawaitaki, na
mwambia Rais Kikwete kuwa Katiba hii hatuikubali,” alisema Maalim
Seif.
Maalim
Seif alisema Katiba bora ni ile inayozingatia maoni ya wananchi.
“Lakini
Rais (Rais Jakaya Kikwete), Katiba yenu mmeweka upande maoni ya
wananchi, mmejifungia wenyewe, mmeipitisha wenyewe na mmeichezea ngoma
wenyewe”, alisema.
Naibu
Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui, alisema wajumbe saba wa Bunge
Maalum la Katiba waliopiga kura ya Hapana hadharani kukataa rasimu hiyo
ni mashujaa wa Zanzibar na Wazanzibari wote wanapaswa kuwapa heshima
kubwa.
Mkurugenzi
wa Habari na Uenezi wa CUF, Salum Bimani, alisema wananchi wa Zanzibar
wameshaamua na hawatarejea nyuma zaidi ya kuiondoa CCM mwaka 2015 na
kuipa Zanzibar mamlaka kamili.
Bimani alisema msiwape kura viongozi wa CCM ambao wanauza nchi ya Zanzibar huku wakicheza ngoma.
“Kwa
Shilingi 300,000 watu hawa wanadiriki kuuza nchi, hawa waliopiga kura
za ndiyo ni madalali wa Zanzibar, hata wale waliopiga kura za siri pia
ni madalali,” alisema Bimani.
Alisema wanasheria wawili wameitetea Zanzibar na wakafikwa na masahiba mazito.
Aliwataka wanasheria hao kuwa Jaji Walfgong Dourado na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyefutwa kazi, Masoud Othman Masoud.
Bimani
alisema Wazanzibari wapo pamoja nao katika kuhakikisha Zanzibar inabaki
na wale wenye nia mbaya wajue kwamba Zanzibar wataitapika watake
wasitake.
Mansour alisema naendelea kuwa muumini wa Maridhiano ya Zanzibar. Katiba hii ni yao wenyewe si ya Wazanzibari.
“Baada ya kuona umma huu uliohudhuria katika mkutano huu tunapaswa kumhofia Mwenyezi Mungu,” alisema.
“Naendelea
kumuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad, ni kiongozi asiyekuwa mnafiki
anajitambua na hatawaliwi na utawala wa Dodoma, anatawaliwa na
Wazanzibari wenyewe na matakwa na matumaini yao,” alisema na kuwataka
Wazanzibari wasiwe na hofu kwani hawawezi kufungwa wote wako wengi sana,
wakati umefika.
“Tumeungana
kwa hiari yetu, tukakubali kwa hiari yetu, sisi si watumwa wa mtu
yoyote, tumefungwa tumefukuzwa makazini kwa sababu ya nchi hii, hatuwezi
kurudi nyuma,” alisema.
Alieleza
kuwa watu wasishangae kumuona Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Mzee
Nassoro Moyo, amesimama kwenye jukwa anatetea nchi yake.
Mzee Moyo alisema Wazanzibari hawakubalini kuona watu wanataka kuichukua nchi yao ovyo ovyo.
Mkutano
huo ambao ni wa kwanza kuhutubia na Maalim Seif tangu BMK limalize kazi
yake na kuwasilisha rasimu kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar,
Dk. Ali Mohammed Shein, ulihudhuriwa na maelefu ya wananchi huku baadhi
yao wakibeba mabango.
Baadhi
ya mabango hayo yalibeba ujumbe usemao “Wapige mabomu rasimu yao
hatuitaki, Hongera Othman Masoud, Katiba ya vijisenti (Chenge)
hatuitaki”.
Katika
hatua nyingine, Maalim Seif alikanusha taarifa kwenye mitandao kuwa
hatajiuzulu wadhifa huo na ataendelea kukiongoza CUF kushika madaraka na
kushika Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika uchaguzi mkuu wa mwakani,
akiwa kwenye nafasi hiyo.
Maalim
alisema taarifa zilizoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa baada ya
kufukuzwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Masoud Othman Masoud, naye
amejiuzulu Umakamu wa Kwanza ni uzushi mtupu.
CHANZO: NIPASHE