Mada Maugo (kushoto) akichuana na Kaseba katika pambano lao la kwanza April 16, 2011 |
Wanamasumbwi hao walipambana mara ya mwisho April 16, 2011 na Maugo kuibuka kidedea kwa TKO ya raundi ya saba baada ya wapambe wa Kaseba kuingia ulingoni na kumvua bondia wao glovu ikiwa bado raundi moja kabla ya pambano hilo kumalizika.
Akizungumza na MICHARAZO hivi punde, Kaseba alisema pambano hilo litakuwa la kuwania taji lililo wazi la WBF kwenye ukumbi kati ya Diamond Jubilee au PTA na litasimamiwa na Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Tanzania (PST).
Kaseba alisema anaamini pambano hilo ndilo litakalomaliza ubishi kati yake na Maugo baada ya kutoridhishwa na ushindi aliopewa walipoumana mara ya mwisho.
Bondia huyo aliyetoka kumnyuka Mmalawi, Rasco Simwanza kwa KO ametamba kuibuka na ushindi mbele ya Maugo ambaye kwa sasa yupo katika maandalizi ya kwenda Russia kuzipiga na mwenyeji wake Movsur Yusupov Julai 27 kwa sababu amebaini ili kumaliza ubishi ni lazima ashinde kwa KO kitu alichoanza kutumia sasa katika mapambano yake.
"Nimebaini ukimpiga mtu kwa KO hakuna malalamiko tofauti na kumaliza pambano na kushinda kwa pointi, hivuo Maugo ajiandae kukumbana na KO ya hatari kwa vile kiu yangu ni kutwaa ubingwa wa dunia kama nilivyofanya kwenye Kick Boxing," alisema Kaseba.
Maugo mwenyewe hakupatikana kueleza tambo hizo za mpinzani wake, ingawa imefahamika kuwa tayari kila kitu juu ya pambano hilo ikiwemo kusainishwa kwa mikataba kumeshafanyika.