|
Zitto Kabwe kati kati na wasanii wa Leka Dutigite |
|
Ali Kiba na Diamond ambao wanadaiwa hawaivi, japo Kiba amekanusha taarifa hizo akidai hana 'bifu' na Diamond |
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, amejitosa kusuluhisha ugomvi wa muda mrefu wa wasanii wawili wa muziku wa kizazi kipya nchini, Ali Kiba na Nasibu Abdul 'Diamond'.
Zitto alitoa kauli hiyo juzi wakati akihojiwa katika Kipindi cha Mkasi kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha EATV baada ya kuulizwa kuwa ni jitihada gani amezifanya kusuluhisha ugomvi wa wasanii hao akiwa kama mlezi wa wasanii wanaotoka mkoani Kigoma.
Alisema anafahamu kuwapo kwa ugomvi wa kutoelewana kati ya wasanii Ali Kiba na Diamond na kwamba alishawahi kufanya jitihada za kuwaita kila mmoja kwa nyakati tofauti.
Alifafanua kuwa katika kuhakikisha anawasuluhisha wasanii hao, anaifanya kazi hiyo kwa umakini kwa sababu hataki kuonekana anaingilia maisha ya watu na kwamba ana imani atafanikiwa kuwapatanisha.
Kuhusu madai kwamba ana uhusiano wa kimapenzi na msanii Mwasiti Almas, alisema ni kweli kumekuwapo na uvumi huo lakini kimsingi hana uhusiano wowote wa kimapenzi na msanii huyo.
"Nasikitishwa na madai hayo yanayotolewa na baadhi ya watu, Mwasiti ni kama dada yangu ambaye nimekuwa nikimsaidia katika kazi zake, kuhusishwa naye kimapenzi ni jambo linalonisononesha,"alisema.
Zitto alisema wanaomhusisha katika suala la mapenzi na msanii huyo ni kwa sababu Mwasiti ameimba wimbo ambao amemtaja yeye (Zitto) lakini kiukweli hana uhusiani naye wa kimapenzi.
Alipoulizwa ni lini ataoa, alisema bado 'yupo yupo' na kwamba kuna mwanamke aliyemtaja kwa jina la Jack ambaye amezaa naye mtoto ambaye kwa sasa miaka nane na anasoma darasa la pili nchini Uganda.
Zitto alizungumzia pia kampuni ya Leka Dutigite inayounganisha wasanii wa Kigoma All Stars, na kusea kuwa ni kampuni ambayo kila msanii anayetoka mkoani Kigoma ana hisa na ikipata faida wanagawana.
Zitto alisema Leka Dutigite pia inamiliki kampuni nyingine ambayo imekuwa ikipata kazi mfano katika Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na yeye kama mlezi amekuwa akitoa fedha zake kusaidia.