NA SULEIMAN MSUYA
ZAIDI ya Wajasiriamali 200 kutoka katika mikoa
mbalimbali ya Kanda ya Ziwa wameshiriki mafunzo ya jinsi ya kuandaa
bidhaa kabla ya kuingia sokoni yaliyoandaliwa na kampuni ya Usalama
Chakula na Ubora (Food Safety and Quality Consultancy Co. Limited)
jijini Mwanza.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni
hiyo Petronella Mlowe wakati akizungumza na mwandishi wa habari kwa njia
ya simu akiwa mkoani Mwanza.
Mlowe alisema katika mafunzo hayo
yaliyofanyika jana na leo jijini Mwanza yamepata mafanikio makubwa kwa
kuwepo kwa mwitikio kwa wajasiriamali wakiume zaidi ya wanawake.
Alisema
pamoja na mwitikio mkubwa kutoka kwa wajasiriamali amebaini kutokuwepo
kwa elimu ya kutosha kwa wahusika wa mafunzo hayo hasa kwenye maandalizi
ya bidhaa jambo ambalo amesema kuwa ni muhimu serikali ikatumia vyombo
vyake kuwajengea uwezo wajasiriamali.
“Mafunzo yamekuwa ya mafanikio
makubwa sana hasa kwa wanaume wengi wamejitokeza jambo ambalo limenipa
matumaini ya kuendelea na kampeni hii ambayo ina lengo la kukuza uchumi
wa wa wajasiriamali wa Kitanzania”, alisema.
Mkurugenzi huyo alisema
mafunzo hayo yalishirikisha wajasiriamali kutoka mikoa ya Mwanza,
Shinyanga, Bukoba na Geita ambapo waliomba kampuni hiyo kuendelea na
mpango huo ili kuhakikisha kuwa wanapata mafanikio.
Alisema
wajasiriliamali wengi ni wale ambao wanajihusisha na uuzaji wa asali,
maembe, chili, pilipili na bidhaa nyingine mbalimbali ambazo zimekuwa
zikiuzwa katika soko la ndani ila la nje hazipatikani.
Pia alitoa
wito kwa asasi, taasisi na mashirika mengine ambayo yanajihusisha na
kuelimisha kutoa elimu ya jinsi ya kuandaa bidhaa hasa katika kuweka
lebo ili kuhakikisha kuwa ubora wa bidhaa unapatikana ili kuleta
ushindani wa ndani na nje ya nchi.
Mlowe alisema kampuni yao
itaendelea kushirikiana na wajasiriamali ambapo zoezi hilo linaendelea
katika mkoa wa Dar es Salaam kuanzia tarehe 28 hadi 29 mwezi huu lengo
likiwa ni kuhakikisha kuwa wajasiriamali wanapata uelewa mzuri juu ya
uandaji wa bidhaa.
No comments:
Post a Comment