|
Sajuki enzi za uhai wake nilipomtwanga picha nyumbani kwake Magomeni kwa Macheni |
KWA kipindi cha miaka miwili mfululizo, Juma Juma Kilowoko maarufu kama Sajuki, aliweza kupigana na kupambana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua tangu mwaka 2010.
Pamoja na kwamba alianza kuugua tangu mwaka 2010, hakuna aliyekuwa anafahamu kutokana na kufanya usiri mkubwa akijiuguza mwenyewe na familia yake, lakini mambo yalipomzidi ndipo mapema mwaka jana alijitokeza hadharani na kuweka bayana kabla ya Mei kupelekwa India kufanyiwa upasuaji.
Tangu alipotoka India, kila aliyemuona kwa siku za karibuni aliamini amefanikiwa kuyashinda mauti, kwa vile alijichanganya na kuendelea na shughuli zake, lakini kumbe Mungu alikuwa na siri kubwa nyuma ya matukio yake kwani alimpa fursa ya kuuaga salama mwaka 2012 na kuuona mwaka mpya wa 2013 kabla ya saa chache akamchukua na kutuachia majonzi watanzania walio wengi.
Sajuki, mmoja wa waigizaji, watunzi, waongozaji na wazalishaji wa filamu nchini aliyekuwa mtu wa watu amesaliwa saa chache kabla ya kupelekwa kwenye makazi yake ya milele katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar er Salaam baada ya kuaga dunia jana asubuhi hospitalini Muhimbili.
Binafsi nilipata taarifa hizo nikiwa nyumbani kwangu, KImara King'ongo nikijiuguza Malaria na mafua makali yaliyonishika tangu Desemba 31 mwaka jana.
Nilishtuka kwa vile zilikuja ghafla mno, japo nilikuwa nafahamu Sajuki, alikuwa kalazwa Muhimbili baada ya kuzidiwa alipokuwa kwenye ziara ya kuwashukuru Watanzania na kuchangisha fedha za kupelekwa tena India jijini Arusha.
Sikuwa na kitu kingine cha kusema zaidi ya Alhamdulillah kulingana na mafundisho ya dini yetu na kumalizia kwa Innalillah Wainaillah Rajiun, kama Mtume Muhammad SAW aliyotuelekeza kila tunapokumbwa na Msiba tuseme hivyo kwa maana kwamba 'Sisi ni waja wa Mwenyezi Mungu na kwake hakika tutarejea'.
Pamoja na kwamba Sajuki ametutoka tungali tukimuhitaji katika fani yake na namna alivyokuwa akionyesha anavyothamini kazi kuliko hata afya yake, lakini Mungu ana mapenzi zaidi na tunapaswa kumshukuru.
Namkumbuka Sajuki, aliyenidokeza jina hilo lilitokana na muunganiko wa majina ya kaka yake aitwae Salum na lake la Juma na lile la ukoo yaani Kilowoko na kuzaa SAJUKI, kwa ucheshi, utani na kujiamini kupita kiasi alikojaliwa na maanani.
Mara ya kwanza kukutana naye nakumbuka ilikuwa mwaka 2009 nyumbani kwake Magomeni Mapipa nilipoenda kufanya mahojiano naye ambapo aliweza kuweka bayana ndoto aliyokuwa nayo tangu utotoni ya kuja kuwa muigizaji mchekeshaji kama Amri Athuman maarufu kama King Majuto.
"Nilitamani sana kuwa mchekeshaji kama King Majuto, lakini filamu za Sylvester Stallone 'Rambo' na ubabe wake zilibadilisha upepo na kujikuta kwenye filamu za kawaida na hasa zile za mapugano na ubabe," aliniambia nilipozungumza naye huku jirani yake akiwepo Soud Ally maarufu kama Chomba au Akuhi.
Sajuki, ambaye majina yake kamili ni Juma Juma Issa Kilowoko, alisema hamu yake ya kufika mbali katika sanaa ya uigizaji ndiyo iliyomfanya apite kundi moja hadi jingine hadi kuangukia Kaole Sanaa, lililomtangaza vema kupitia michezo iliyokuwa ikirushwa na kituo cha runinga cha ITV.
Alisema mchezo wake wa kwanza ndani ya kundi hilo lililotoa nyota kibao wa filamu nchini ni Baragumu wa mwaka 2005 na kufuatia na michezo mingine hadi mwaka 2008 alipojitoa kundini na kujikita zaidi katika filamu, kazi yake ya kwanza ikiwa ni Revenge.
"Baada ya kupita makundi kadhaa tangu nikiwa mjini Songea nilipozaliwa, hatimaye nilitua Kaole Sanaa, lililoniivisha kabla ya kuachana nao kusaka masilahi zaidi na kujikita katika filamu," alisema.
Mbali na Revenge filamu zingine alizocheza Sajuki ni pamoja na Dhambi, Mboni Yangu, Two Brothers, Behind the Scene, Round, Shetani wa Pesa, Hero of the Church na nyinginezo.
Wakati nilipokuwa nazungumza naye alikuwa akijiandaa kutoa filamu mbili binafsi za Vita na Briefcase zilizowashirikisha nyota kadhaa nchini akiwemo mshindi wa pili wa BBA, Mwisho Mwampamba.
Sajuki alisema fani ya filamu imemnufaisha kwa mambo mengi ikiwemo kimaisha, lakini kubwa ni kufanikiwa kumuoa mke mrembo na muigizaji mwenzake, Wastara Issa Juma 'Stara'.
"Kufanikiwa kumpata Wastara na kumuoa kwangu ni jambo kubwa na la kuvutia mno kati ya mafanikio kibao niliyoyapata katika fani hii ya filamu nchini," alisema.
Mkali huyo, aliyekuwa akipenda kucheza na watoto na shabiki wa muziki wa 'Quito', alisema kama kuna kitu kinachomkera katika sanaa hiyo ni tabia za 'Wauza Sura' wanaojiingiza kwenye skendo chafu zinazowachafua wasanii wote wa tasnia hiyo mbele ya jamii.
Alisema wasanii wenye kusaka umaarufu kwa lazima wanamnyima raha kwa vile jamii inadhani wasanii wote wana silka na tabia kama za wauza sura hao wanaojirahisi na kujidhalilisha.
Kuhusu rushwa ya ngono, Sajuki mtoto wa nne kati ya watano wa Mzee Juma Issa Kilowoko, alisema wanaojihusisha nao wanafanya hivyo kwa kujitakia kwa sababu hakuna anayelazimishwa kutoa mwili wake iwapo ana uwezo na kipaji kikubwa katika sanaa hiyo.
"Rushwa ya ngono kwa watoto wakike ni kujitakia kwa vile wana akili na ufahamu wa kujua athari za kufanya hivyo na watayarishaji wanaolazimisha hawafai na wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria," alisema Sajuki.
Sajuki, alinidokeza kuwa hakuna kitu kilichomtia simanzi na kumsikitisha kama tukio la ajali ya pikipiki iliyompata akiwa na mkewe, Wastara Juma enzi wakiwa wachumba.
Nyota huyo ambaye ameacha mjane na mtoto mmoja wa kike, aliishukuru familia yake na Vincent Kigosi 'Ray' kwa kumfikisha alipokuwapo alisema ajali hiyo sio inayomuuma, ila kitendo cha kulazimika kuidhinisha fomu hospitalini ili Wastara akatwe mguu wake uliokuwa umeharibika kwa ajali hiyo.
"Kwa kweli kile kitendo cha kuidhinisha kukatwa kwa mguu kwa Wastara kinaniuma hadi leo, lakini sikuwa na jinsi ila kufanya hivyo ili kumuokoa," Sajuki aliniambia kwa masikitiko katika mahojiano hayo.
Hata hivyo alidai alikuwa akijisikia fahari mno kuoana na kisura huyo ambaye kwa sasa anao mguu wa bandia, kwa vile wamesaidiana kuanzisha kampuni yao binafsi ya Wajey Films Production.
Sajuki alizaliwa miaka 27 iliyopita huko Songea na kusoma hadi elimu ya sekondari katika shule za Songea na Luwiko, alikoanza kuonyesha kipaji chake cha sanaa katika matamasha mbalimbali ya shule kabla ya kujitosa kwenye makundi.
Mungu ailaze mahali pema roho ya marehemu Sajuki anayezikwa kesho katia makaburi ya Kisutu.
Mwisho