Kado akitambulishwa na viongozi wa Coastal Union hivi karibuni |
KLABU za Yanga na Mtibwa Sugar
zimeendelea kuzozana kuhusiana na mchezaji Shaaban Kado baada ya kipa huyo
kusaini mkataba wa kuichezea Coastal
Union ya Tanga kwa mwaka mmoja.
Kipa huyo ambaye aliichezea Mtibwa kwa
mkopo katika mzunguko wa kwanza wa msimu akitokea Yanga, amekuwa chanzo cha
malumbano baina ya klabu hizo; ambapo ‘Wanajangwani’ wanadai kuwa wana haki ya
kumuuza kokote kwavile ni mchezaji wao halali huku ‘wakata miwa’ wa Mtibwa
wakisisitiza kuwa anapaswa kuendelea kubaki kwao kwavile walimtwaa kwa mkataba
wa kuichezea hadi mwisho wa msimu.
Hata hivyo, akizungumza jana, Kado alisema kuwa tayari ameshasaini
mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Coastal iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu
ya Tanzania Bara mwaka 1988.
“Ni kweli nimesaini mkataba wa mwaka
mmoja katika klabu ya Coastal… na nimeshaanza kufanya nao mazoezi,” alisema
Kado.
Akieleza zaidi, kipa huyo alisema:
“Kulikuwa na mvutano kati ya Yanga na Mtibwa juu yangu, lakini kila kitu
kuhusiana na hilo nimewaachia wao. Naamini watamalizana,” alisema Kado.
Mratibu wa Mtibwa, Jamal Bayser, alisema jana kuwa wameshangazwa na kitendo cha Yanga kumuuza mchezaji huyo
il-hali walikubaliana kuichezea timu yao (Mtibwa) hadi mwishoni mwa msimu huu
wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Bayser alisema kuwa tayari klabu yake
imewasilisha malalamiko katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusiana na
suala la kipa huyo ambaye aliwahi kuichezea Mtibwa kabla ya kuuzwa Yanga na
baadaye kurejea tena klabuni hapo kwa mkopo.
“Inashangaza sana kuona klabu zinasajili
wachezaji kinyume na utaratibu. Kulingana na makubaliano yetu na Yanga, Kado
anatakiwa kuitumikia Mtibwa hadi mwishoni mwa msimu huu,” alisema Bayser.
“Tumeshaandika barua TFF, maana
tulikubaliana na na Yanga, tena tukaweka mkataba kimaandishi. Sasa tunasubiri
TFF watoe maamuzi,” aliongeza mratibu huyo.
Alipotafutwa na gazeti hili jana
kuzungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kuwa
kwa sasa hawana muda wa kuzungumzia suala hilo kwavile Kado si mali yao tena
kwa sasa.
“Kado ni mali ya Coastal Union kwa sasa,
siwezi kuzungumzia suala la mchezaji huyo maana siyo mali yetu tena (Yanga),”
alisema Mwalusako.
Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura
alisema kuwa sakata la mchezaji huyo limepelekwa kwenye Kamati ya Sheria, Maadili
na Hadhi za Wachezaji ya TFF ili lipatiwe ufumbuzi.
Chanzo:NIPASHE
No comments:
Post a Comment