Carlos Tevez |
Nyota huyo wa zamani wa West Ham United, Manchester United na Manchester ity amekuwa nje ya kikosi hicho cha taifa tangu 2011 alipocheza mechi ya kichapo cha robo fainali ya michuano ya Copa America dhidi ya Uruguay.
Hata hivyo, kocha mpya Gerardo Martino, ambaye alichukua mikoba kutoka kwa Alejandro Sabella kufuatia kipigo cha mechi ya fainali ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Ujerumani, alisema mapema mwezi huu kuwa milango iko wazi kwa Tevez kurejea kikosini kama atathibitisha ubora wake katika ngazi ya klabu.
Na sasa kocha huyo wa zamani wa Barcelona amemuita kikosini nyota huyo (30) kwa ajili ya mechi za kuwakabili Ureno na Croatia, kufuatia kufunga magoli nane katika mechi 10 akiwa na Juventus msimu huu.
Miongoni mwa wakali walioitwa yupo nahodha Lione Messi, mshambuliaji Sergio Aguero, Angel di Maria, Javier Mascherano, Marcos Rojo, Pablo Zabaleta, Martin Demichelis, huku pia Erik Lamela wa Tottenham naye akiitwa siku chache tu tangu alipofunga goli "la miujiza" la mkasi wa kupiga mpira kwa kupitisha mguu wa kushoto nyuma ya mguu wa kulia.