KINYANG'ANYIRO cha Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kinaanza leo kwa pambano la kukata na shoka baina ya vinara wa Ligi ya Hispania, Atletico Madrid dhidi ya kikosi cha Jose Mourinho \,Chelsea ya England.
Atletico imetamba imejijiandaa kumshangaza Mourinho leo katika mechi hiyo baada ya kumzuia kumaliza msimu wake wa mwisho nchini Hispania bila kombe.
Mourinho ataiongoza Chelsea leo kucheza hatua ya nne bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Calderon dhidi ya Atletico inayoongoza msimamo wa La Liga ikiwa ni mara ya kwanza timu hizo kukutana nusu fainali kwa kipindi cha miaka 40.
Mourinho alitolewa na Borussia Dortmund katika raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2012-13, wakati na Real Madrid huku msimu huo Barcelona ikiutwaa ubingwa wa La Liga na kisha kulikosa Kombe la Mfalme (King’s Cup) katika mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Bernabeu dhidi ya Atletico.
Bao la kichwa la Miranda katika muda wa nyongeza lilikifanya kikosi cha Diego Simeone kuibuka na ushindi wa 2-1 katika mechi hiyo ya fainali ambayo Mourinho na mshambuliaji Cristiano Ronaldo walitolewa nje kwa kadi.
"Uhitaji kuwa mtabibu kueleza kuwa matokeo ya fainali hayakuwa ya haki, kuwa Atletico si washindi tu," Mourinho aliuambia mkutano wa wanahabari baada ya mechi hiyo.
Tukirudi Chelsea, kwa sasa Mourinho anahitaji kulipa kisasi huku akitaka kuweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu tatu tofauti baada ya kutwaa ‘ndoo’ hiyo wakati akiinoa Porto 2004 na Inter Milan 2010.
Yeye na kikosi chake cha Chelsea atakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Atletico ambayo inaongoza msimamo wa La Liga ambayo inakaribia kuutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza tangu 1996, ikiwa na Simeone ambaye ameshatwa La Liga na Kombe la Mfalme mara mbili.
Atletico itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata mwishoni mwa wiki kwenye La Liga dhidi Elche, wakati Chelsea yenyewe ikiwa na huzuni ya kulala 2-1 nyumbani dhidi ya Sunderland, hicho kikiwa ni kipigo cha kwanza cha Mourinho Stamford Bridge katika mechi 78.
Mourinho alikataa kujibu maswali baada ya mechi na kuonekana akimlaumu zaidi mwamuzi kuliko wachezaji wake, akidai ameiua Chelsea, jambo ambalo limepunguza kasi zao za mbio ubingwa.
"Wamefanya kila kitu walichotaka," aliuambia mkutano wa wanahabari.
"Walipigana, kucheza kuanzia mwanzo hadi mwisho wa pili na walistahili hilo (alisifu)," aliongeza kocha huyo mwenye umri wa miaka 51.
"Mara nyingine tunawatukuza wakati tunaposhinda lakini nadhani ni sahihi kuwapongeza wachezaji wangu baada ya kipigo."
Kulikuwapo na hofu kama kipa wa Atletico, Thibaut Courtois, ambaye anaichezea klabu hiyo kwa mkopo akitokea Chelsea, angecheza mechi ya leo dhidi ya timu yake, lakini Simeone alisema baada ya mechi dhidi ya Elche kwamba nyota huyo wa Kimataifa wa Ubelgiji atajumuishwa.
Mbali na sakata hilo la mkopo, klabu hizo mpili zilikubaliana kuwapo kwa penalti ya kiasi cha fedha endapo Atletico itamchezesha Courtois dhidi ya Chelsea lakini Shirikisho la Soka barani Ulaya (Uefa) limesema makubaliano hayo ni kinyume na sheria za mashindano hayo.
"Hakuna yeyote aliyezungumza lolote na mimi, hivyo kama ilivyo atacheza," alisema Simeone.
Kipigo kwenye Kombe la Mfalme ndicho pekee kilichomkuta Mourinho katika rekodi yake dhidi ya Atletico, kwani mara zingine nane walizokutana alishinda.
Hata hivyo, Atletico ni timu pekee katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo haijafungika na imeshinda mechin zake zote tano ilizocheza nyumbani ikiwa ni pamoja na dhidi ya mabingwa wa zamani AC Milan na Barca.
Mshindi wa jumla wa mechi hiyo na pindi zitakaporudiana, atacheza fainali dhidi ya Real Madrid ama Bayern Munich katika mchezo wa fainali utakaopigwa Lisbon, Ureno.
Hatua nyingine ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya itaendelea kesho kati ya Bayern Munich na Real Madrid ambayo imepata ahueni baada ya Cristiano Ronaldo kupona majeraha yaliyokuwa yakimsumbua na hivyo kuanza kujifua kwa ajili ya mechi hiyo.