MWENYEKITI
wa Baraza la Wazee wilayani Kilolo, Lunyiliko Nyaulingo amelazwa katika
Hospitali ya mkoa Iringa na Mwenyekiti wa CHADEMA Mgololo amelazwa
Hospitali ya wilaya ya Mufindi baada ya kujeruhiwa vibaya na watu
wanaodaiwa ni wanachama wa CCM katika kampeni za mwisho za kuwania
nafasi ya udiwani.
Sambamba na hiyo Katibu wa CCM kata ya
Ng’ang’ange wilayani Kilolo, Wilhad Ngogo (40) na Yohana Mchafu
anayedaiwa kuwa ni mwanachama wa CCM wanashikiliwa na Polisi kwa
kuhusika na matukio hayo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema watu hao walikamatwa jana kufuatia
vurugu zilizojitokeza kwenye mikutano ya kampeni ya mwisho katika wilaya hizo mbili.
Alisema
kufuatia mzozo huo wanachama wa CHADEMA walizuia barabara ya
Iringa-Mbeya kwa kuweka magogo ili kuzuia magari kupita na kuwa Polisi
wanamtafuta Rabart Sam maarufu kwa jina la Kideri kwa kuongoza vurugu
hizo.
Kamanda Mungi alisema wanafanya uchunguzi wa kina juu ya matukio hayo na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
Aidha
alitoa wito kwa viongozi wote wa vyama vya siasa kufanya kazi kwa
mujibu wa sheria ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza kutokea.
Leo
Uchaguzi wa udiwani katika kata ya Ng’ang’ange wilayani Kilolo na
Mbalamaziwa wilayani Mufindi ulifanyika ambapo Zuberi Nyomolelo (CCM) na
Ezekiel Mlyuka (CHADEME) walipambana kwa kata ya Mbalamaziwa na kwa
upande wa Ng’ang’ange Kilolo Nafred Chahe (CHADEMA) na Namgalesi Msuva
(CCM) walipambana.
Tukio hilo limejiri wakati huko Morogoro nako inaelezwa wanaodaiwa vijana walinzi wa CCM kuwakata mapanga viongozi wa CHADEMA, huku watanzania wakiendelea kuomboleza tukio la mlipuko wa bomu jijini Arusha lililopoteza uhai wa watu wawili na wengine kadhaa kujeruhiwa.