Kikosi cha Golden Bush Veterani |
TIMU ya soka ya Golden Bush Veterani, leo inatarajiwa kushuka dimbani kupepetana na wapinzani wao, Wahenga Fc ikitaka kulipiza kisasi cha kipigo ilichopewa na wapinzani wao hao katika mechi ya kuuaga mwaka 2012.
Golden Bush, ilikumbana na kipigo cha aibu kwa kunyukwa mabao 4-3, licha ya kuchezesha nyota kadhaa wa zamani wa timu za Simba, Yanga na Mtibwa Sugar na waliomba mechi hiyo ya marudiano ichezwe leo kama mechi ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2013 na kusherehekea miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka wa maeneo ya Sinza na vitongoji vyake kutokana na vijembe vilivyokuwa vimetawala tangu baada ya mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita na Wahenga kuwazidi maarifa wenzao na kulipa kisasi cha kipigo walichowahi kupewa na wapinzani wao hao.
Wahenga walinyukwa mabao 4-2 katika pambano lililochezwa katikati ya Oktoba, wiki moja baada ya kutoka sare ya baoa 1-1 katika mechi zote zilizochezwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa TP Sinza.
Pande mbili za timu hizo wamekuwa wakitambiana kwamba leo ndio mwisho wa mzizi wa fitina, Golden Bush wakiapa lazima warejeshe kipigo hicho walichopewa na Wahenga walichokilalamikia kilichangiwa na maamuzi ya 'kimamluki' yaaliyokuwa yakifanywa na mwamuzi, Ally Mayay Tembele.
Mlezi wa Golden Bush, Onesmo Waziri 'Ticotico' alisema kuwa kikosi chao kimejiandaa vya kutosha kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa majira ya jioni kwenye uwanja wa TP, huku akiwahimiza mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia watakavyoishindilia mabao Wahenga.
"Tutakachofanya leo ni kujumlisha idadi ya mabao tuliyofungana mechi iliyopita, yaani 4+3 na idadi yake ndiyo ambayo Wahenga watakavyobeba kipigo hicho, tupo fiti na mie mwenyewe natarajia kusaidia safu ya mashambulizi kwa sababu jamaa wamechonga sana baada ya kutuotea Desemba 31," alisema Ticotico.
Hatari katika lango la Wahenga, Golden Bush siku walipotoka sare ya bao 1-1. Je leo nani atakayecheka au kulia? |
No comments:
Post a Comment