Na Rahma White
LIMEBAKI kama saa moja na ushei tu kabla ya Simba na Azam kumaliza ubishi kwenye pambano la fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017 litakalopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar.
Simba inacheza fainali yake ya sita katika msimu huu wa 11 wa michuano hiyo, ilihali Azam itakuwa ni ya tatu, lakini ikiwa na rekodi ya kusisimua ya kuingia fainali chache lakini haijawahi kuacha taji.
Iliingia mwaka 2012 na 2013 na mara zote likabeba taji mbele ya Jamhuri ya Pemba na KCCA, wakati Simba katika fainali zake tano za awali imetwaa mara tatu ikiwa klabu yenye historia ya kutwaa mara nyingi taji hilo.
Licha ya rekodi hizo za kusisimua kwa wababe hao wa Ligi Kuu Bara, bado timu yoyote itakayocheza vema na kutumia kwa ufanisi dakika 90 inaweza kubeba taji na kuhitimisha siku 15 za michuano hiyo iliyoanza Desemba 30, 2016.
Makocha na wachezaji wa timu zote wamekuwa wakitambiana tangu walipofahamu watakutana kwenye mchezo huo utakaoanza majira ya Saa 2:15, lakini ukweli ni kwamba lolote linaweza kutokea usiku huu visiwani humo.
Simba inayotarajiwa kupanga kikosi karibu chote kilichoitoa nishai Yanga kwa kuifunga kwenye nusu fainali, inaivaa Azam ikiwa haijkapoteza mechi yoyote ila imeruhusu bao moja wavuni wake, tofauti na Azam ambayo haijafungwa kabisa.
Mbali na mashabiki usiku kutaka kushuhudia timu ipi itakuwa bingwa mpya wa michuano ya mwaka huu, pia fainali hizo zitakuwa na utamu mwingine wa kujua wachezaji gani watakaonyakua tuzo za Ufungaji Bora, Kipa Bora, Mchezaji Bora Chjipukizi na Mchezaji Bora wa michuano.
Mpaka sasa tuzo ya Mfungaji Bora ni kama inarudi tena kwa Simon Msuva aliyetwaa mwaka 2014 akiwa na mabao manne sawa na aliyonayo msimu huu, licha ya timu yake ya Yanga kutolewa.
Wachezaji waliokuwa wakimfukuzia winga huyo mchachari, Bokota Labama wa URA Uganda ma Abdulsamad Kassim wa Jang'ombe Boys timu zao zimeaga michuano, japo Laudi Mavugo mwenye mabao mawili anaweza kumvurugia.
Kipa Bora nafasi ipo wazi kwa Aishi Manula wa Azam ambayo mpaka timu yake ikiivaa Simba, hajaruhusu bao lolote na akiwa ameonyesha kiwango cha hali ya juu, huku Daniel Agyei wa Simba naye aliyeibuka shujaa katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Yanga kwa kuokoa penalti mbili za Deo Munishi 'Dida' na ile ya Haji Mwinyi anaweza kujikuta akibeba, iwapo Simba itafanya yake usiku huu.
Kwenye tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi ni vigumu kufahamu kwa sasa kwa sababu kuna vijana wengi walioonyesha makali akiwamo Enock Atta-Agyei wa Azam ambaye ndio kwanza anamiaka 18, lakini amepiga soka la nguvu Zanzibar.
Bila shaka ni suala la kusubiri kujua mambo yatakuwaje na MICHARAZO MITUPU litakuletea hatua kwa hatua ya pambano hilo mpaka mwisho wa fainali hiyo, usiache kuperuzi blog yako makini upate uhondo.
No comments:
Post a Comment