STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 28, 2015

Ghana, Algeria watinga robo fainali, vumbi jingine leo

Andre Ayew akichuana na mchezaji wa Bafana Bafana
Wachezaji wa Algeria wakishangilia ushindi wao dhidi ya Senegal
VINARA wa soka Afrika, Algeria na Ghana zimefuzu hatua ya Robo Fainali ya michuani ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON), kwa kishindo baada ya kuziondosha patupu timu za Senegal na Afrika Kusini katika mechi zao za mwisho za Kundi C zilizochezwa katika miji ya Malabo na  Mongomo.
Algeria walikuwa wametoka kuduwazwa na Ghana kwa kufungwa bao 1-0 katika mechi yao iliyopita, walipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya waliokuwa vinara wa kundi hilo la kifo, Senegal katika pambano tamu lililochezwa kwenye uwanja wa Malabo.
Ikiwa bila nyota wake Islam Slimani, Algeria wanaoongoza orodha ya viwango vya soka barani Afrika waliwashtukiza wapinzani wao kwa bao la mapema la dakika ya 11 lililowekwa kimiani na Riyad  Mahrez lililodumu hadi wakati wa mapumziko.
Senegal walicharuka kusaka kurudisha bao hilo ili angalau waambulie sare na kuwavusha hatua hiyo ya mtoano, lakini walijikuta wakikatishwa tamaa baada ya Algeria kuandika bao la pili dakika nane kabla ya kumalizika kwa pambano hilo baada ya Nabil Bentaleb kumalizia kazi nzuri ya
Sofiane Feghouli.
Kwa kipigo hicho Senegal wameyaaga mashindano hayo sambamba na Afrika Kusini ambayo ilikumbana na kipigo cha mabao 2-1 toka kwa Ghana waliokuwa nyuma hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Bafana Bafana iliyofuzu fainali hizo kwa kishindo bila ya kupoteza mchezo katika kundi lake lililokuwa na waliokuwa mabingwa Nigeria, ilianza kupata bao katika dakika ya 17 kupitia kwa Mandla Masango, lakini katika kipindi cha pili waliruhusu wapinzani wao kurejesha bao hilo na kuongeza jingine lililowapeleka robo fainali bila kutarajiwa baada ya kuianza michuano hiyo kwa kichapo cha mabao 2-1 toka kwa Segenal.
Bao la kusawazisha la Ghana liliwekwa kimiani na John Boye katika dakika ya 73 baada ya kuunganisha mpira wa krosi ya Andre Ayew 'Pele' kabla ya mtoto huyo wa nyota wa zamani wa Afrika, Abeid Pele kufunga bao la ushindi kwa kichwa katika dakika ya dakika ya 83 na kuwavusha mabingwa hao manne wa michuano hiyo katika hatua hiyo ya robo fainali.
Ghana imemaliza kileleni mwa kundi hilo wakilingana pointi sita na Algeria waliokamata nafasi ya pili, huku Senegal wameshika nafasi ya tatu wakiwa na pointi nne na Bafana Bafana wameburuza mkia wakivuna pointi moja tu.
Hatua ya robo fainali inatarajiwa kuanza kuchezwa siku ya Jumamosi kwa pambano la kukata na shoka baina ya majirani Congo-Brazzaville dhidi ya DR Congo kabla ya Tunisia kuvaana na wenyeji Guinea ya Ikweta katika pambano jingine la pili.
Ghana na Algeria zenyewe zinatarajiwa kushuka dimbani siku ya Jumapili kumenyana na washindi wa kundi D ambalo usiku wa leo zibnatarajiwa kuumana kuwania nafasi mbili zilizobaki za kutinga hatua hiyo ya robo fainali.
Wakati Ivory Coast na Cameroon zitaumana kwenye uwanja wa Malabo, wenzao Mali na Guinea watapepetana kwenye uwanja wa Mongomo, huku timu zote zikiwa na nafasi sawa kutokana na kulingana kila kitu wakiwa na pointi mbili baada ya kila moja kucheza mechi mbili.

No comments:

Post a Comment