MCHEZAJI mkongwe wa mpira wa kikapu nchini Marekani, Michael Jordan 'Air Jordan' ameendelea kuweka rekodi katika vitabu hata baada ya kustaafu mchezo huo baada ya kutajwa kama mwanamichezo pekee aliyechomoza katika orodha ya mabilionea ulimwenguni.
Wakati akicheza kikapu katika ligi maarufu nchini Marekani NBA, Jordan aliweka rekodi mbalimbali kutokana na umahiri pindi anapokuwa uwanjani lakini hali hiyo imebadilika kwani hivi sasa ameonyesha kuwa mahiri kibiashara pia.
Jordan mwenye umri wa miaka 52 ametajwa kushika nafasi ya 1,741 katika orodha ya watu matajiri duniani ambayo hutolewa na jarida la Forbes kila mwaka akiwa mwanamichezo pekee kuchomoza katika orodha hiyo.
Nguli amepata utajiri mkubwa kutokana na kuingia mkataba na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike ambao ulimuingizia zaidi ya dola bilioni 2.25 mwaka 2013 pamoja na kumiliki hisa asilimia 89 zenye thamani ya dola milioni 700 katika timu ya Charlotte Hornets.
No comments:
Post a Comment