STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, November 19, 2012

SERENGETI BOYS WANUSA FAINALI ZA AFCON U17


BAO lililotokana na faulo iliyotolewa kwa Serengeti Boyz na refa Mganda Miiro Nsubuga baada ya Hussein Ibrahim wa Serengeti kuchezewa faulo na beki wa Congo, Mohendik Brel iliisaidia timu ya Tanzania U17 kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kongo jana.
 

Mfungaji wa bao hilo alikuwa kiungo Mudathir Abbas, aliyekwamiza faulo hiyo dakika ya 15 na kuiwezesha Serengeti Boys kushinda bao 1-0 na kujiweka katika nafasi nzuri  ya kufuzu fainali za Afrika mwakani zitakazofanyika nchini Morocco.

Pambano la timu hizo lilifanyika jana kwenye uwanja wa Taifa na kushuhudia vijana wa Serengeti Boys wakikaribia kurejea rekodi iliyowekwa na kaka zao wa timu hiyo mwaka 2004 walipotinga fainali kabla ya kung'olewa kwa kosa la kuchezesha 'kijeba' Nurdin Bakar.

Bao hilo pekee la Sengereti lilipatikana dakika mbili tu baada ya kipa Peter Manyika Peter kudaka vyema mpira wa kichwa uliopigwa na Ibara Vinny kutoka karibu na lango uliokuwa ukionekana kuelekea golini kuitanguliza Kongo mbele.

Wageni waliokuwa wamewazidi 'mno' vijana wa Serengeti kutokana na muonekano wao wa 'miili jumba',  walicharuka baada ya goli hilo na kufanya mashambulizi mfululizo huku wakitawala sehemu kubwa ya mchezo huo ambao ni wazi kuwa matokeo yangekuwa vinginevyo kama si uhodari wa Manyika aliyestahili tuzo ya mchezaji bora wa mechi.

Ushindi uliiweka Serengeti katika mazingira mazuri ya kuandika historia kwa kufuzu kihalali kwa fainali za Afrika kwa mara ya kwanza ikiwa watafanikiwa walau kuambulia sare katika mechi yao ya marudiano itakayochezwa Brazzavile wiki mbili zijazo.

Serengeti waliwahi kufuzu kwa fainali hizo lakini wakaondolewa baada ya kukutwa na hatia ya kuchezesha wachezaji wenye umri mkubwa, lakini safari hii wamepata mteremko na kunusa fainali zitakazofanyika mwakani nchini Morocco baada ya wapinzani wao wa awali kujitoa na sasa kubakiwa na kazi ya kuitoa Congo tu ili itinge kwa fainali hizo.

Basile Erikiki, kocha wa Congo aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu dakika mbili kabla ya kumalizika kwa kosa la kumbwatukia refa akiwa karibu na mstari wa uwanja, aliipongeza Serengeti kwa kuonyesha ushindani mkali na soka la kasi, lakini akijipa matumaini ya kusonga mbele kwa kudai kuwa vijana wake watajirekebisha kwa kutumia vyema nafasi watakazopata katika mechi ya marudiano tofauti na ilivyokuwa jana.

Ticha wa Serengeti, Jacob Michelsen, amewasifu vijana wake kwa kuibuka na ushindi katika mechi aliyokiri kwamba ilikuwa ngumu kwa kila upande.
"Ila bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kutimiza lengo la kuwatoa wapinzani wetu (Congo) na kusonga mbele," alisema Michelsen.

Vikosi: Peter Manyika, Miza Abdallah, Mohamed Mohamed, Ismail Gambo, Miraji Adam, Mudathir Abbas, Mohamed Haroub, Joseph Lubasha/Dickson Ambundo (dk.60), Hussein Ibrahim, Selemani Bofu/Tumaini Mosha (dk. 76) na Farid Shah.

Congo Brazzavile: Ombandza Mpea, Imouele Ngampio, Mabiala Charlevy, Okombo Francis, IOndongo Bowrgema, Ibara Vinny, Binguila Bardry, Obassi Ngatsongo, Mohendiki Brei, Atoni Mavoungou na Biassadila Arci.  

No comments:

Post a Comment