STRIKA
USILIKOSE
Wednesday, September 5, 2012
Erick Mawalla: Kinda anayeililia ligi ya vijana, kombe la Taifa
KUTOKUWEPO kwa ligi ya muda mrefu na ya kudumu kwa timu za vijana na kutopewa kipaumbele kwa michuano ya Kombe la Taifa, kunamfanya beki kinda anayepanda chati nchini, Erick Mawalla 'Sekana' aamini ni sababu ya kudidimia kwa soka la Tanzania.
Beki huyo aliyetua African Lyon akitokea timu iliyoshuka daraja ya Moro United anasema michuano ya timu za vijana na Kombe la Taifa kwa mtazamo wake ndio ukombozi wa soka la Tanzania na kurejesha makali yake katika anga la kimataifa.
"Hatuwezi kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa iwapo hatuna ligi ya vijana, lazima iwepo mipango ya kuanzisha ligi hiyo na kuipa kipaumbele michuano ya Kombe la Taifa, ambayo siku za nyuma ilitumika kuibua nyota waliotamba nchini," anasema.
Anasema hata klabu na mataifa yanayofanya vema katika soka la kimataifa, zilipoteza fedha zao kuwekeza kwa vijana na mavuno yao yanavutia kila mtu, kitu ambacho ametaka Tanzania nayo kufuata nyayo hizo ili ifanikiwe.
"Bila kuwepo kwa ligi ya kudumu ya vijana, au shule maalum za kukuzia vipaji tangu utotoni na kutopewa kipaumbele kwa michuano muhimu kama Kombe la Taifa ni vigumu kuwa na timu imara kuanzia ngazi za klabu mpaka timu za taifa," anasema.
Erick aliyeanza kucheza soka tangu shuleni kama winga kabla ya kubadilishwa na kuwa beki, anasema kuanzia serikali, wafadhili, viongozi na mashabiki watambue hakuna njia ya mkato ya mafanikio katika michezo bila watu kuwekeza fedha zao katika sekta hiyo.
NYOTA NJEMA
Kinda hilo, linalopenda kula chakula cha aina yoyote mradi akimdhuru na kunywa Juisi, anasema anashukuru soka kumsaidia kwa mengi ikiwamo kutwaa mataji na tuzo kadhaa tangu akiwa kinda ukiacha mafanikio binafsi ya kimaisha.
"Siwezi kusema nimefanikiwa sana, ila nashukuru kwa muda mfupi niliopo katika soka nafarajika nimeweza kupata mafanikio ya kujivunia ikiwamo kutwaa vikombe, tuzo na kupata fedha zinazosaidia kuendesha maisha yangu," anasema.
Erick, 'swahiba' mkubwa wa Mfungaji Bora wa michuano ya Super 8 anayeichezea Simba, Edward Christopher 'Eddo Boy', anasema moja ya mataji ambayo hawezi kusahau maishani mwake ni Kombe la Copa Coca Cola 2007 akiwa na timu ya vijana ya Kinondoni.
"Hili ndilo lilikuwa taji langu la kwanza kubwa katika maisha ya soka, kwa hakika nilifurahi mno kuipa Kinondoni taji hilo, ingawa nimeshatwaa pia ubingwa wa Kombe la Taifa nikiwa na Ilala na mwaka jana tulishika nafasi ya tatu katika michuano kama hiyo," anasema.
Erick, aliyeingia kwenye soka kwa kuvutiwa na 'mapacha' wa zamani wa klabu anayoishabikia ya Manchester United, Dwight Yorke na Andy Cole, anasema kabla ya kuibukia kwenye Coca Cola, kipaji chake kilianza kuonekana Kijitonyama Stars aliyoichezea tangu akiwa darasa la sita.
"Baadae nilitua Yanga B nikiwa na swahiba wangu Eddo Boy na wengine, lakini kutokana na klabu hiyo kuonekana haikuwa na mipango endelevu ya soka la vijana, nilihamia Moro Utd B na kuichezea kwa misimu kadhaa akishuka na kupanda nayo Ligi Kuu," anasema.
Chipukizi huyo anasema alikuwa katika kikosi cha Moro kilichoshuka daraja msimu wa 2009-2010 na kuirejesha tena Ligi Kuu msimu uliopita kabla ya kuzama tena na yeye kukimbilia African Lyon.
Matarajio ya Erick anayeishabikia pia Real Madrid na aliyewataja makocha Juma Matokeo na Seleman Kiiza kama watu waliosaidia kukuza kipaji chake, ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi akidai tayari ameanza kipango ya jambo hilo.
"Kiu yangu kubwa ni kucheza soka la kulipwa hasa Ulaya, naamini ni kipaji na uwezo wa kufanya hivyo, ingawa napenda kabla ya hapo nipate fursa ya kulitumikia taifa langu," anasema.
Mchezaji huyo anasema licha ya kuitwa mara kadhaa katika vikosi vya timu za vijana U17 na U20, kiu yake kubwa ni kuichezea Taifa Stars.
NSAJIGWA
Erick anayehuzunishwa na kifo cha baba yake kilichotokea mwaka 2006, anasema licha ya kucheza mechi nyingi, pambano gumu kwake ni lile la Moro United dhidi ya Yanga lililochezwa msimu uliopita na lililoisha kwa sare ya mabao 2-2.
Anasema anaikumbuka mechi hiyo hasa kwa tukio lililofanywa na aliyekuwa nahodha wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa cha kumpiga 'kiwiko' winga wao Benedict Ngassa na kutolewa nje kwa kadi nyekundu na jinsi Yanga iliyosawazisha bao la pili.
"Ni mechi hiyo na ile ya nusu fainali dhidi ya Mwanza katika michuano ya Kombe la Taifa 2011 tuliyopoteza ndizo ninazozikumbuka kwa ugumu na namna zilivyojaa upinzani," anasema.
Erick Lawrance Mawalla alizaliwa Julai 5, 1993 jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa kwanza kati ya wanne wa familia yao, alisoma Shule ya Msingi Bunge kabla ya kutua Makongo Sekondari kutokana na kipaji chake cha soka.
Akiwa Makongo ndiko alikoitwa timu ya vijana ya Kinondoni na baadae timu ya taifa ya U17 kabla ya kupandishwa ile ya U20 chini ya kocha Kim Poulsen.
Anasema kama kuna watu anaowashukuru kumsaidia kufanikiwa kisoka na maisha basi si wengine zaidi ya wazazi, makocha wake na wachezaji wenzake bila kuusahau uongozi wa Moro United.
Erick anayependa kusikiliza muziki na kuangalia filamu, anasema kama angekutana na Rais wau Waziri wa Michezo kilio chake kingekuwa juu ya kujengwa shule maalum za michezo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment