STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, June 25, 2013

Kipemba, Mapigo 7 wahamasisha ulipaji kodi Ujiji-Kigoma


      
Msanii Yasini Mapigo Saba akiwa na Issa Kipemba
    
MUIGIZAJI nyota wa zamani wa kundi la Kaole Sanaa, Issa Kipemba 'Kipemba' akishirikiana na msanii Yassini  Mapigo Saba wa mkoani Kigoma, wameendesha kampeni ya kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa wakazi wa manispaa ya kigoma Ujiji.

Kampeni hizo zilizoambatana na burudani ya ngoma asilia, vichekesho na uigizaji, ziliandaliwa na ofisi ya Manispaa ya mji huo wa Ujiji –Kigoma kupitia mradi wa Tanzania Strategic Cities Project (TSCP) chini ya Mstahiki Meya Bakari Beji.

Alisema alijikuta akishiriki kampeni zilizoambatana na utoaji wa elimu ya ulipaji wa kodi za manispaa hiyo kwa ajili ya kuongeza chachu ya maendeleo alipoenda kwa likizo fupi na kama msanii alijiona ana dhima ya kuisaidia jamii yake.

"Nilikuwa nimeenda kusalimia nyumbani na kukuta uhamasishaji huo na mie kushiriki kama msanii na mwenyeji wa Ujiji na tumefanya kazi kubwa nikishirikiana na msanii mkongwe wa Kigoma, Mapigo Saba," alisema.

Naye mstahiki meya wa manispaa ya Kigoma ujiji  alithibitisha kufanyika kwa kampeni hizo akidai zilikuwa zina lengo la kuchochea hamasa kwa wakazi wa mji huo kujenga tabia ya kulipa kodi zilizopo katika manispaa yao ili kuongeza kasi ya maendeleo ya manispaa yao.

"Ni kweli Kipemba na wasanii wengine akiwamo Mapigo Saba walikuwa hapa kuendesha kampeni ya elimu na uhamasishaji wa ulipaji wa kodi za manispaa na kwa kiasi kikubwa wamefanya kazi kubwa na tunasubiri utekelezaji toka kwa wananchi," alisema  Mstahiki Meya Beji.

Aidha mweka hazina wa manispaa hiyo ndugu Edward Malima alianisha kodi zilizoahamasishwa kwa wananchi wa Kigoma - Ujiji kuwa ni pamoja na kodi za Majengo, Ushuru wa Huduma ya Mji, Maegesho ya magari, Masoko na Vizimba, Hoteli na Nyumba za wageni (guest), na Mabango ya Matangazo.

Ndugu Malima alitilia mkazo kwa kutofautisha kodi za maegesho ya magari na ile ya Stendi za mabasi ambapo alitanabahisha umuhimu wa ulipaji wa kodi hizo kwa ustawi na maendeleo ya mji wa Kigoma Ujiji huku akitoa mifano lukuki ya maendeleo ya sasa ya manispaa hiyo ukilinganisha na hapo nyuma.

No comments:

Post a Comment