STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 3, 2013

Azam yaendelea kuanika sababu za kuing'oa AS FAR Rabat kesho nchini Morocco

Mshambuliaji John Bocco 'Adebayor' akichuana na wachezaji wenzake mazoezini mjini Rabat, Morocco kujiandaa na pambano lao la kesho dhidi ya AS  FAR Rabat

Na Patrick Kahamela, Rabat
SIKU chache zilizopita tulijadili juu ya sababu mbili kati ya sita, kwa nini Azam FC ina nafasi kubwa ya kuibwaga AS FAR, katika, katika makala ya jana tuliangalia jinsi Azam FC ilivyofanya maandalizi kabambe kwa kuijengea timu kujiamini kwa kuipa mechi za majaribio na maandalizi mengine. Baada ya hapo tulijadili jinsi Azam FC ilivyo na wachezaji kabambe wenye uwezo wa kupambana na timu yoyote kwenye mashindano ya Afrika. Tulifanikiwa kuwaangalia wachezaji wa eneo la ulinzi pekee, leo tutawaangaliwa wachezaji wa kiungo na ushambuliaji na sababu nyingine nne zilizosalia zinazoifanya Azam FC iwe katika nafasi kubwa ya kuitoa AS FAR.

Azam FC wakati wa dirisha dogo ilimsajili mchezaji wa kiungo toka SOFAPAKA Ochieng Humphrey Mieno, tangia kuwasili mieno amekuwa habanduki kwenye kikosi cha kwanza na kazi yake nzuri imeiwezesha Azam FC kufikia mafanikio iliyonayo hadi sasa. Mieno ni mrefu kwa kimo, ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, mzuri kwenye kusoma mbinu za adui na kupanga mipango ya kuizima na ana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo wa ushambuliaji na ulinzi. Hakika usajili wa Mieno umekuwa wa maana kubwa kwa Azam FC.

Tanzania kwa sasa inajivunia kuwa na wachezaji wenye kiwango cha juu cha uchezaji na ndiyo maana timu ya taifa imekuwa ikifanya vizuri. lakini ukiwaomba mashabiki wakutajie wachezaji watatu bora zaidi nchini basi bila shaka watakuambia ni Mbwana Samata wa TP Mazembe, Shomary Kapombe wa Simba na Salum Abubakar Sure Boy wa Azam FC. Sure boy amekuwa mchezaji wa kipekee kabisa kwa sasa… uwezo wake wa kupokonya mipira, kumiliki mipira na kuipa timu umiliki wa mpira ni wa hali ya juu sana. Sure Boy anazurura sana uwanjani na hachoki kirahisi. Azam FC inajivunia kumtengeneza mchezaji huyu ambaye alitua Azam FC akiwa na miaka 16 tuu na kwa sasa amekuwa lulu inayong’aa.

Utawaambia nini mashabiki juu ya Sure? Utawaambia nini wachezaji wenzake? Muulize kocha wake juu ya Sure, wote watakuambia ni mchezaji wa dunia yake na wa kipekee. Hakika silaha kubwa ya Azam FC kesho ni Salum Abubakar.

Azam FC imejaaliwa kuwa na wachezaji wengi wa kiungo lakini Jabir Aziz Stima ana sifa ya kipekee inayomfanya kuwa mchezaji muhimu kikosini. Stima ambaye alikuwa hakosekani kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Marcio Maximo ni mchezaji pili wa Afrika baada ya Dedier Drogba kuweza kuifunga Brazil goli, je ulikuwa unalijua hilo? Stima alifuga wakati Stars ilipocheza na Brazil na kufungwa 4-1 kwenye mchezo wa kirafiki mwaka 2010. Stima ni bingwa wa kukaba. Kocha wake Stewart Hall anamuita mbwa wa polisi, muingize Stima uwanjani kisha mwambie akakabe kisha uone kama wapinzani wataweza kupiga zaidi ya pasi tano. Katika mchezo wa kesho ambao ni wa ugenini… Stima anatarajia kuwa na sehemu muhimu.

Sifa za kukaba za Stima pia anazo muaiverikosti Kipre Michael Bolou na hii inaifanya Azam FC iwe na uwigo mpana wa kupanga kikosi. Kocha akitaka wakabaji basi atawapanga Jabir Aziz na Kipre Bolou, lakini akitaka kucheza mpira basi atawatumia Abdi Kassim, Humphrey Mieno, Sure Boy na Mwaipopo. Wachezaji wote hawa wamesafiri na wapo katika hali nzuri. Ni suala la kusubiri tuu kuona nini kitatokea hiyo kesho.


Kipre Bolou alisajiliwa wakati wa dirisha dogo la msimu uliopita baada ya pacha wake kipre tchetche kuonesha mafanikio makubwa. Tangia awasili kipre Bolou amekuwa mhimili mkuu wa eneo la ulinzi. Amecheza karibu mechi zote na ilipobidi alifunga magoli mazuri sana. Azam FC inajivunia kuwa na mchezaji wa kimataifa wa aina ya Kipre Bolou.


Baadhi ya wachezaji wa Azam wakipasha nchini Morocco
Baadhi ya msafara wa Azam ukiwasilia Rabat, mbele ni Patrick Kahemela na kocha Stewart Hall
Ibrahim Joel Mwaipopo ni mmoja kati ya wachezaji waliosajiliwa na Azam FC mara baada ya kupanda ligi kuu misimu minne iliyopita. Mwaipopo mchezaji anayetumia zaidi mguu wa kushoto amekuwa akicheza kwenye eneo la kiungo cha ulizi na kazi yake imekuwa ya uhakika kiasi cha kumfanya kuwa na mkataba wa muda mrefu na Azam FC. Mwaipopo ana jicho la kuona nafasi, ana pasi za uhakika fupi na ndefu lakini pia anajua kupiga mashuti yenye macho. Ukiomuona mazoezini utaamini kuwa anakwenda kuanza kesho lakini ukimkuta anaanzia bechi huta shangaa kutokana na aina ya wachezaji ambao Azam FC inao kwa sasa.

Abdi Kassim Babi ni mchezaji mzoefu zaidi kwenye kikosi cha Azam FC na siku hizi amekuwa na uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa kati au kurudi kwenye eneo lake la kiungo na kucheza kama namba kumi. Babi ana uzoefu wa mashindano ya ngazi hii na uzoefu wake unatarajia kuisaidia sana Azam FC hapo kesho. Ukitafuta wachezaji wa kiungo wa Tanzania watano wenye uwezo mkubwa wa kufunga na kupiga mipira ya adhabu basi hutaacha kumtaja Abdi kassim.

UONGOZI BORA WENYE BENCHI BORA LA UFUNDI NA MIPANGO NA DHAMIRA YA USHINDI


Azam FC ina uongozi bora na makini chini ya bodi ya wakurugenzi inayoongozwa na management ya Bakhresa Group, uongozi wa Azam FC chini ya mwenyekiti Said Muhammad ulichukua kila tahadhari kwa ajili ya mchezo huu ikiwemo kutanguliza timu ya watu saba kufanya ushushushu wa mazingira yalivyo na maandaliza kabla timu haijawasili. Mashushushu hao waliuarifu uongozi umuhimu wa kuwahi na Azam FC iliandika barua TFF kuomba mechi yale na Coastal Union irudishwe nyuma ili kuweza kuwahi Rabat. Azam FC iliwasili Rabat siku sita kabla ya mchezo kuweza kufanya mazoezi kwa zaidi ya mara nane ili kuzoea hali ya hewa ya baridi kali iliyopo hapa.
 
Pia klabu ilinunua nguo za michezo za kuvaa kwenye baridi kwa ajili ya wachezaji, soksi nzito za miguuni na mikononi, fulana za kukaba za kuvaa ndani pamoja pamoja na raba za kushindia ili kuondoa sababu za hali ya hewa kuweza kuathiri maandalizi ya timu na uwezo wa timu uwanjani.


Azam FC inakaa kwenye hotel ya nyota tano ya Golden Tulip Farah hapa Rabat hii inawafanya wachezaji wasiwe na manung’uniko na wasiathirike kiasaikolojia kutokana na matatizo ya huduma. Viongozi wamekuwa wakihakikisha timu inapata kila inachohitaji na hadi sasa hakuna tatizo lolote lililojitokeza.


BENCHI LA UFUNDI
Azam FC ipo chini ya kocha Stewat Hall, huyu ni mwalimu wa kiwango cha juu sana akiwa anamiliki cheti cha ukocha cha UEFA PRO LICENCE inayomfanya kuwa mkufunzi wa makocha kule uingereza.



Makocha wa Azam, Waingereza John Stewart Hall na Kally Ongalla
  
Stewart Hall kwa kushirikiana na wasaidizi wake wamepata nafasi si tuu ya kuangalia mikanda ya video ya AS FAR waliyotafutiwa, lakini pia wamepata nafasi ya kuwaangalia AS FAR ‘live’ wakiwa uwanjani na hii inawapa uelewa zaidi na kubuni mbinu za kuwakabili.


Azam FC imekamilika na imekuja na timu kamili akiwemo kocha mkuu Stewart Hall, wasaidizi wake Kalimangonga Ongala na Iddi Abubakar, Mtunza vifaa Joseph Nzawila, Meneja Jemedary Said na Daktari Juma Mwanandi Mwankemwa. Hakika timu imejipanga na ina hamu ya kushinda na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya soka.

No comments:

Post a Comment