Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas |
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema jana kuwa Anita ambaye ni mkazi wa Usa River wilayani Arumeru, alivamia kituo cha M-Pesa kinachomilikiwa na Stela Mrema akiwa na mwanamume mmoja.
Alisema watu hao wanaodaiwa kuwa ni majambazi, baada ya kufika kwenye kituo cha huduma hiyo maeneo ya Shamsi jijini hapa majira ya saa 6:00 mchana wakijifanya wateja, ghafla mmoja wao (Anita) alichomoa bastola kwenye mkoba wake na mwenzake akatoa bunduki na kuamrisha wapewe fedha.
“Baada ya kuingia walijifanya kuhitaji huduma ya M-Pesa, ghafla yule mwanamke alitoa bastola kwenye mkoba wake na mwanaume naye alitoa bunduki na kuwaamuru watoe pesa na simu… ndipo yule mteja alimpiga kichwa yule mwanamke na kisha kupiga kelele za kuomba msaada hivyo walifanikiwa kumdhibiti,” alisema.
Hata hivyo, alisema mwenzake alifanikiwa kukimbia. Alisema baada ya polisi kumtaka Anita awataje wenzake, polisi waliwakamata watuhumiwa wanne waliokuwa wamepanga kufanya uporaji huo.
Kamanda Sabas aliwataja waliokamatwa kuwa ni Abdulahman Jumanne Idd (27) ambaye ni mwangalizi wa Kampuni ya Ulinzi ya KK na mkazi wa Shamsi, Simon Martine au Mapanki (45) mkazi wa Kwa Mrombo, Hashimu Ally (30) ambaye ni mpanda milima na mkazi wa Ngarenaro na Charles Luangano (24) ambaye pia ni mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya KK.
Alisema watuhumiwa hao baada ya kufanyiwa upekuzi walikamatwa na bunduki aina ya shotgun, bastola aina ya bereta na risasi sita za bastola. Alisema watafikishwa mahakamani Jumatatu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment