STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 10, 2012

Peter Manyika: 'Straika' wa zamani anayefuata nyayo za baba yake









HANA muda mrefu tangu alipotumbukia katika soka, lakini kipaji kikubwa cha alichonacho cha soka kimeanza kumtabiria kuja kuwa nyota kama baba yake aliyewahi kung'ara na timu za Mtibwa Sugar, Yanga na Taifa Stars.
Peter Manyika, ndiye kipa namba moja kwa sasa wa timu ya taifa ya vijana ya U17 'Serengeti Boys' iliyozikosa kiduchu fainali za Afrika zitakazochezwa mwakani nchini Morocco baada ya kujikwaa kwa vijana wenzao wa Kongo.
Manyika, mtoto wa kwanza wa nyota wa zamani, Manyika Peter ndiye aliyekaa langoni katika mechi zote dhidi ya Kondo ikiwemo ile ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani na kipigo cha mabao 2-0 ugenini wiki iliyopita.
Kipa huyo anasema mechi ya pili dhidi ya Kongo ndiyo mechi itakayobaki kichwani mwake kama tukio la huzuni kwa kushindwa kuisaidia Serengeti Boys kurejea tukio la mwaka 2004 kufuzu fainali za Afrika kabla ya kutolewa.
Manyika aliyeanzia kucheza kama mshambuliaji wa kati kabla ya kubadilishwa namba akiwa Shule ya Msingi, baada ya kipa wao kuumia na yeye kuhamishiwa langoni na kung'ara, anasema vurugu walizofanyiwa Kongo hatazisahau.
"Kwa kweli fujo na vitimbi tulivyofanyiwa Kongo ni mambo yanayonifanya nishindwe kuisahau mechi hiyo kwani hatukutarajia kama tungerudi salama kwa namna walivyotufanyia 'unyama' ndani na nje ya uwanja," anasema.
Manyika, anayetarajiwa kuibukia timu ya U20 ya Mgambo Shooting katika michuano ya Kombe la Uhai baada ya kuachana na  JKT Ruvu, anasema kwa tukio la furaha hakuna kama alipoitwa timu ya taifa na kuwa kipa namba moja.
"Sio siri kuitwa kwangu Serengeti Boys kulikuwa kwa kushtukiza sikutarajia na furaha zaidi ni kuwa kipa namba moja wa timu hiyo," anasema.
Manyika anasema japo anajiamini ana kipaji cha soka cha kuzaliwa na kurithi toka kwa baba yake, lakini hakutarajia mafanikio hayo ya mapema.

CASILLAS
Manyika anayemtaja mjomba wake, David 'Mzee wa Yeah' na Method kama walioibua na kukiendeleza kipaji chake kabla ya baba yake kutia nguvu, anasema alivutiwa kisoka na nyota wa zamani wa Brazil, Ronaldo de Lima na kujikuta akicheza kama mshambuliaji wa kati.
Anadai hata hivyo alipohamia kwenye ukipa amehamisha mapenzi kwa kipa Joe Hart na Ike Casillas aliyedai ndiyo kiigizo chake huku akimzimia pia Yew Berko wa Yanga.
Manyika anayependa kula ugali kwa dagaa na mlenda na kunywa Fanta, anadai japo Ronaldo kastaafu soka bado anaendelea kuwa mchezaji bora kwake kuwahi kumuona kutokana na umahiri wake wa kufumania nyavu.
Akiwa na ndoto za kucheza soka la kulipwa, Manyika anayesoma kidato cha tatu kwa sasa katika Shule ya Sekondari Kizuka iliyopo Morogoro, anasema kipindi kifupi alichokuepo katika soka amenufaika kwa mambo mengi.
Anadai kutumainiwa na taifa, kumudu maisha kwa kujinunulia vitu bila kutegemea wazazi na kusafiri sehemu mbalimbali ni baadhi ya mafanikio hayo.
Manyika anasema donge nono kulipata ni Sh 540,000 alizopata hivi karibuni na kutumia kununua godoro, runinga na deki yake na matumizi mengine.
"Nashukuru fedha hizo zimenifanya niwe kila kitu cha kuanzia maisha kwani mama yangu alinichongea pia kitanda. Huwezi amini awali hakupenda kabisa nicheze soka ila kwa sasa ananiunga mkono," anasema.

NDOTO
Manyika anayezishabikia Yanga, Barcelona na Real Madrid akiwazimia Dimitar Babatov na Ronaldo, anasema japo Serengeti Boys imeshindwa  kufuzu fainali za Afrika anadhani itafanya hivyo baadaye.
Pia anasema anaamini Taifa Stars chini ya Kim Poulsen ikijipanga vema inaweza kufuzu fainali za Kombe la Dunia na za Afrika kwa vile kocha huyo ni mjanja, mjuzi na mwenye malengo mazuri.
"Kim nimefanya naye kazi ni bonge la kocha na watanzania tunapaswa kumuunga mkono na kumkumbatia kwani anaweza kutupeleka mbali, hata fainali za Dunia, muhimu tujipange, japo watu wanaona ni ngumu."
Manyika anayemtaja John Bocco kama nyota anayemzimia Bongo, anadai wakati anaibukia katika soka hakutaka kabisa kutumia mgongo wa baba yake mpaka alipogundua kama amejitosa kwenye mchezo huo.
"Huwezi amini aliyenisaidia kufika hapa ni mjomba wangu Mzee Yeah, baba alikuja kuwa msaada wa kuninunulia vifaa baada ya kutambua nimejitosa kurithi kipaji chake."
Anaongeza kwa kuwashukuru wawili hao, pia mama yake kipenzi, Method na, ndugu, jamaa na rafiki wote wanaomuunga mkono.

KIPAJI
Peter Manyika 'Casillas' alizaliwa Agosti 13, 1996 jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa kwanza kati ya wawili wa familia yao, elimu yake ya Msingi aliisoma Shule ya Rutihinda kabla ya kujiunga na Kizuka Sekondari.
Kisoka, alianza makeke yake tangu shule ya msingi akicheza kama 'straika'  kabla ya kuhamia kwenye ukipa, timu yake ya kwanza ya kueleweka ikiwa ni Zaragoza ya Magomeni kabla ya kutua kituo cha soka cha Twalipo.
Anasema akiwa na kituoni hapo mwaka jana aling'ara katika michuano ya Airtel akiichezea Shule ya Jitegemee kisha kutua JKT Ruvu U20 na kuichezea katika Kombe la Uhai.
Baadaye Juni mwaka jana aliitwa Serengeti Boys na kumudu nayo mpaka sasa na hivi karibuni ameelekea Mgambo Shooting U20 atakaoicheza katika michuano ya Uhai 2012.
Akiowa na ndoto za kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa, Manyika hutumia muda wake wa ziada kusikilia muziki, kuangalia muvi na anadai soka la Bongo  lipo juu hasa baada ya vijana kupewa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.
Anasema kama hali hiyo ikiendelea Tanzania itafika mbali, japo ametaka wadau wa soka kuwekeza zaidi na kudhamini klabu zote bila ubaguzi pia akitaka kuongezeka kwa michuano mingi zaidi ya ile ya ligi.
Juu ya Simba na Yanga, kinda hilo linalowasihi wachezaji wenzake kuzingatia mazoezi na kulitumaini soka kama ajira zao zinazoweza kuwatoa kimaisha anasema hana papara za kuzikimbilia kwa vile anataka kwanza kujenga jina.
"Simba na Yanga kwa sasa ni kubwa mno kwangu, labda baadaye tena kwa kuridhishwa na masilahi, napenda zaidi kucheza nje ya nchi au klabu isiyo na presha kubwa kama vigogo hao," anasema.

No comments:

Post a Comment