STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, March 16, 2013

Yanga bila Yondani kuivaa Ruvu Shooting leo

Wachezaji wa Yanga wataendelea kushangilia mabao leo kwa Ruvu kama hivi?

VINARA wa Ligi Kuu nchini Yanga chini ya Kocha wake, Ernst Brandts wanatarajiwa kushuka dimbani jioni ya leo kuvaana na Ruvu Shooting, bila beki wake mahiri wa kati, Kelvin Yondani.
 Hata hivyo Brandts amesema licha ya kumkosa beki huyo, bado anaamini Yanga itaibuka na ushindi katika mechi hiyo itakayochezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Yanga wanaongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 45 baada ya mechi 19 wakifuatwa na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam (37) na mabingwa watetezi wa Simba walio katika nafasi ya tatu (34).
Akizungumza jana baada ya kumalizika kwa mazoezi ya timu yake kwenye uwanja wa Bora wa Kijitonyama, jijini Dar es Salaam jana, Brandts alisema atawatumia mabeki waliopo kuziba pengo la beki huyo tegemeo kwa Yanga na timu ya taifa, 'Taifa Stars'.
Hata hivyo, ni wazi kwamba safu ya ulinzi ya Yanga haipo vizuri kwa sasa kutokana na kukosekana kwa mabeki watatu.
Ladislaus Mbogo ni mgonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji wa uvimbe shavuni, Yondani anasumbuliwa na tatizo la uvimbe wa kidole gumba cha mguu na Stephano Mwasika ana maumivu ya misuli ya mguu.
“Naamini tutacheza vizuri licha ya kuwakosa mabeki wetu hao kwa sababu wachezaji wengine wako safi kiafya, kiakili na wana morali ya hali ya juu katika kuhakikisha timu inapata ushindi katika mechi ya Jumamosi (leo),” alisema Brandts.
Ruvu Shooting inayonolewa na Boniface Mkwasa inakamata nafasi ya saba katika msimamo wa ligi hiyo baada ya kucheza mechi 18, na imekuwa na historia ya kuikamia Yanga katika mechi baina yao.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, Yanga waliokuwa nyuma kwa magoli mawili hadi mapumziko, walizinduka na kuibuka na ushindi wa 3-2 katika kipindi cha pili.
Tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu Januari 26, Yanga ambao ni mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, wameshacheza mechi sita wakishinda tano na kutoka sare moja.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa Sh. 5,000, Sh. 8,000, Sh. 15,000 na Sh. 20,000, kwa mujibu wa taarifa ya shirikisho la soka (TFF).

No comments:

Post a Comment