STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, February 2, 2014

Bwana Misosi mkali anayeaminia 2014 ni mwaka wa wazoefu wa muziki Bongo

 
WAKATI ngoma yake mpya ya 'Vuta Raha' aliyoimba akimshirikisha msanii chipukizi Namcy, msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya Joseph Rushahu maarufu kama 'Bwana Misosi' anajiandaa kutoa kazi nyingine mpya akitamba mwaka 2014 ni mwaka wa wakongwe kurejea kwenye chati.
Mkali huyo aliyejihusisha na sanaa tangu akiwa kinda kabla ya kujitosa jumla mwaka 1995, anasema wakongwe wanataka kurejesha heshima ya muziki wa kizazi kipya kwa tungo zenye mafunzo kwa jamii, mbali na zile za kuburudisha.
Hata hivyo mkali huyo aliyejipatia umaarufu mkubwa kupitia nyimbo zake mbili zilizofuatana za 'Nitoke Vipi' na 'Mabinti wa Kitanga', anasema cha muhimu 'media' ziwape sapoti za kutosha kwani bila ya vyombo vya habari ni vigumu dhamira yao kufanikiwa.
"Media itutendee haki kwa kutupa 'airtime' kama ilivyo kwa wasanii wanaoibuka sasa, kisha waache mashabiki wapime wenyewe, kwa sasa wakongwe ni kama tunasahauliwa kwa kazi zetu kutopewa nafasi kwenye redio na runinga kama wasanii wapya," anasema.
Misosi  aliyokimbiza kwa albamu ya 'Nitoke Vipi' ya mwaka 2004 na ile ya Kazi Yangu ya mwaka 2007 anasema bado wakongwe wana mchango mkubwa kwa jamii kupitia nyimbo zao hivyo wapewe nafasi sawa na wasanii wapya hata kama ni kweli 'kila nabii ana zama yake'.
Misosi katika pozi jingine
MKALI
Misosi aliyevutiwa kisanii na nyota wa zamani wa kimataifa wa Marekani, 2Pac kuonyesha alivyo mkali kutupitia tungo zenye akili waliwahi kunyakua tuzo ya Kili Music-2009 kupitia kibao chake matata cha 'Mungu Yupo Bize' aliomshirikisha Said Chege.
Mbali na wimbo huo mkali huyo ambaye hivi karibuni alitumbukia kwenye fani ya filamu alishatoa vibao vingine kadhaa kama  'Heshima' aliyomshirikisha Mkenya Red Sun, 'Huwezi Jua' aliyoimba na Jua Cali pia wa Kenya, na 'Nimesomeka'’ aliomshirikisha Nikki Mbishi.
Pia amekimbiza na nyimbo nyingine kali kama 'Pilato na Game' alioimba na Sir Juma Nature na Fid Q na Iweje, iliyoutangulia 'Vuta Raha'.
Misosi  anasema amekuwa akitoa kazi baada ya kipindi kirefu kwa vile alikuwa 'bize' na masomo  pamoja na kusoma alama za nyakati hivyo kulazimika kujipanga vyema kabla ya kutoa kazi ili kuendelea kubamba mashabiki.
"Soko la muziki kwa sasa limebadilika, hivyo watu hawapaswi kukurupuka, sitaki kufanya kazi kwa mazoea ndiyo maana nimekuwa nikiachia ngoma kila baada ya kipindi fulani," anasema.
Mkali huyo anasema kwa sasa hana mpango wa kutoa albamu kama zamani kutokana na wizi uliokithiri unaofanywa na maharamia kwa kazi za wasanii na kuwaacha wasanii wasinufaike na jasho lao huku taifa likipoteza mamilioni ya fedha kama wangeiwekea mipango mizuri ya kuvuna kodi.
"Ningekutana na Rais ningemweleza mengi, ila moja ni juu ya sanaa yetu, jasho tunalomwaga ni tofauti na kipato tunachopata."
Anasema kama angekuwa Rais angetoa kipaumbele kwa sekta za kijamii kama Afya na Elimu pamoja na sanaa na michezo ili kusaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.

SOKA
Misosi anayependa kula wali kwa samaki rosti na kunywa Fanta Orange, anasema kama siyo kunogewa na muziki, huenda angekuwa mmoja wa nyota wa soka kutokana na kuupenda mchezo huo tangu akiwa kinda.
Anasema mbali na kuupenda soka amelicheza akimudu nafasi za namba 7, 8 na 9 na kuzichezea timu kadhaa zilizokuwa Ligi Daraja la Nne mjini Tanga kama Maumau, Roma na Central Paris.
"Nadhani ningeendelea kukomalia soka, ningefika mbali pengine kuvaa jezi ya timu ya taifa kwa kipaji kikubwa nilichonacho katika mchezo huo, ila nadhani Mungu alinifungulia neema yangu iwe kwenye muziki," anasema.
Misosi anayezishabikia klabu za Yanga, Barcelona na Chelsea, anasema japo amejikita kwenye muziki lakini siku moja moja hujikumbushia soka kwa vile ni mchezo anaoupenda kwa dhati.
Mkali huyo, anasema hakuna tukio la furaha maishani mwake kama kukubalika kwake na kazi zake mbele ya mashabiki wa muziki ndani na nje ya nchi, huku akisikitishwa na vifo vya baba yake Gabriel Rushahu na cha kaka yake Emmanuel Rushahu kilichotokea hivi karibuni.
Misosi katika pozi
ALIPOTOKA
Misosi anachekelea muziki kumpa mafanikio mengi kimaisha ikiwamo umaarufu unaomrahisishia baadhi ya mambo yake, japo hajaridhika mpaka afike mbali zaidi na kurejesha shukrani kwa jamii, alizaliwa mwaka 1980.
Elimu yake ya Msingi aliisoma Mwanga, Kilimanjaro na ile ya Sekondari aliipatia katika Shule ya Popatral ya Tanga ambako ndiko alikopewa jina hilo la 'Bwana Misosi' kutokana na tabia yake ya kupenda kulakula.
Tangu akiwa shuleni Misosi, alijihusisha na michezo na sanaa akimudu kucheza soka, sarakasi, kuigiza, kupiga ngoma na kupuliza filimbi.
Anasema licha ya kipaji cha kuzaliwa, alijikuta akitamani kuwa msanii kutokana na kuvutiwa na 2Pac ndipo mwaka 1995 alipojitosa rasmi katika fani hiyo kabla ya kuja kutoka miaka ya 2000 alipotoa kazi zilizomzalishia albamu mbili tofauti.
Msanii huyo ambaye pia ni mjasiriamali na anayependa kutumia muda wake kuogolea, kusafiri, kuangalia muvi, soka na ngumi 'live', anakiri kwamba muziki Bongofleva umepiga hatua kubwa kulinganisha na siku za nyuma.
Hata hivyo anapenda wasanii wenzake kuongeza ubunifu ili uzidi kushika kasi, anamshukuru Mungu, familia yake na mashabiki wake kumfikisha hapo alipo.
Amewataka wasanii wenzake kupendana, kushirikiana na kuisaidia kwa shida na raha huku akiwasisitiza umuhimu wa kujiheshimu na kujithamini mbele ya jamii.

No comments:

Post a Comment