STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 29, 2012

Mwalala aamua kutundika daluga, kisa maumivu wa nyonga

Ben Mwalala alipokuwa Yanga

MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa timu za Yanga na Coastal Union, Ben Mwalala, ameamua kutundika daluga na kujikita kwenye ukocha kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya muda mrefu ya nyonga.
Akizungumza na MICHARAZO leo jijini Dar es Salaam, Mwalala aliyewahi kung'ara na timu za Mumias ya Kenya,  Sc Villa ya Uganda na APR Rwanda, alisema maumivu hayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu na ndiyo yaliyomuondoa Coastal Union msimu huu.
Mwalala aliyeichezea Yanga kwa nyakati tofauti kati ya kwa 2006-2009, alisema kwa vile ana mapenzi makubwa na soka ameamua kuendeleza mchezo huo kwa kujikita kwenye ukocha akiwa tayari ameshachukua mafunzo ya awali na ngazi ya kati mpaka sasa.
"Kaka nyonga imenifanya nistaafu soka ningali kijana, hata hivyo bado sijatoka katika katika mchezo huo kwani nimeamua kusomea ukocha ili kuendeleza jahazi na hivi karibuni nimetoka kumaliza kozi za ngazi ya kati iliyoendeshwa na TFF," alisema.
Mwalala aliongeza, mipango yake ni kusomea kozi ya ngazi ya juu ya ukocha wa soka kisha kuja kuwa mwalimu wa timu yoyote itakayokuwa inamhitaji.
Mkenya huyo, ambaye 'amelowea' nchini, alisema anaamini bado ana mchango mkubwa katika soka ndani na nje ya nchi ndio maana imekuwa vigumu kwake kuacha moja kwa moja mchezo huo.
Mwalala anakumbukwa na mashabiki wa Yanga kwa kusaidia kufuta uteja wa miaka nane iliyokuwa nayo klabu hiyo mbele ya watani wao wa jadi, Simba kwa bao pekee alililofunga katika mechi ya kwanza ya msimu wa 2008 iliyoichezwa Oktoba 26.
Pia alikuwa mmoja wa walioifungia  Yanga mabao mawili yalioipa sare ya 2-2 katika mechi ya marudiano na watani zao hao iliyochezwa uwanja wa Taifa, Aprili 19, 2009.

No comments:

Post a Comment