STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, December 30, 2011

Matumla alilia ushindi kwa Maneno, mratibu ampuuza




BINGWA wa zamani wa Dunia wa Ngumi za Kulipwa, Rashid Matumla 'Snake Man', ameibuka na kudai alistahili kuwa mshindi wa pambano lake dhidi ya Maneno Oswald 'Mtambo wa Gongo' lililofanyika Desemba 25 jijini Dar es Salaam.
Pia bondia huyo amewalalamikia waandaaji wa mchezo huo kwa madai ulingo ulikuwa una utelezi, kiasi cha kumfanya aanguke mara kadhaa na kupelekea kuumia mkono na mguu.
Katika pambano hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa Heinkein Pub, Mtoni Kijichi, Matumla na Maneno walishindwa kutambiana baada ya kutangazwa wametoka sare kwa kupata pointi 99-99, kitu ambacho Maneno alikipinga akidai alistahili yeye ushindi.
Hata hivyo, Matumla naye ameibuka na kudai yeye alistahili kutangazwa mshindi kwa namna alivyocheza na kumdhibiti mpinzani wake aliyekiri ni mmoja wa mabondia wazuri nchini.
"Kwa kweli licha ya kwamba mwamuzi na majaji ndio watu wa mwisho katika maamuzi na kukubaliana na maamuzi ya kutangaza droo baina yangu na Maneno, lakini naamini nilistahili kuwa mshindi kwa jinsi nilivyocheza," alisema Matumla.
Matumla, alisema hata baadhi ya mashabiki waliofurika kwenye ukumbi huo walikuwa wakilalamikia droo iliyotangazwa kitu kinachoonyesha mechi ile haikustahili kuwa hivyo.
Pia, alisema kuanguka kwake mara kwa mara ulingoni kulitokana na ulingo kuwa na utelezi na kutoa ushauri wa waandaaji wa ngumi wawe wakiepuka vitu kama hivyo ili kusaidia kufanya mabondia waonyeshe uwezo wao na kuwapa burudani mashabiki.
"Waandaaji wawe makini na maandalizi ya michezo yao, wajaribu kuandaa ulingo wenye ubora sio kama ilivyotokea katika pambano letu ambapo kulikuwa na utelezi na kusababisha niumie mkono na miguu kwa kuanguka wakati wa mchezo,"alisema.
Muandaaji wa pambano hilo, Shaaban Adios 'Mwayamwaya' ameyapinga madai ya Matumla kwa ulingoni ulikuwa na utelezi kwa kudai kuwa ulingo huo kwa miaka mingi ndio 'Snake Man' amekuwa akiutumia kuwapiga wapinzani wake.
Adios alisema ulingo huo uliletwa na DJB Promotion, ambao ndio waliowakodisha na juu ya kuanguka kwa Matumla, alisema alimueleza viatu vyake vilikuwa vimelika 'kashata'.
"Kama ulingo ulikuwa unateleza mbona Maneno hakuwa akianguka, pia ndio ulingoni mkubwa na wenye ubora wa hali ya juu kati ya ulingo zote nchini na ambao Matumla amekuwa akiutumia kuwapiga wapinzani wake," alisema Adios.

Mwisho

No comments:

Post a Comment