STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, September 13, 2011

Hammer Q aibuka Eagle Modern taarab



MUIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Husseni Mohammed 'Hammer Q' ameanzisha kundi jipya la miondoko hilo, liitwalo Eagle Modern Taarab 'Wana Kimanumanu' likiwa limeshaachia nyimbo mbili mpya za kulitambulisha.
Akizungumza na Micharazo, Hammer Q, alisema kundi hilo linaloundwa na wasanii 16, linajiandaa kukamilisha albamu yao ya kwanza itakayokuwa na nyimbo tano, mbili kati ya hizo zimerekodiwa video na zimeshasambazwa ili virushwe hewani.
Hammer Q aliyekuwa Five Star baada ya awali kulitema kundi la Dar Modern Taarab, alizitaja nyimbo zilizorekodiwa audio na video kwa ajili ya kulitambulisha kabla ya kuanza kufanya maonyesho yake ni Tatu Bila na Zangu Dua.
"Baada ya kimya kirefu, nimeibuka nikiwa na kundi jipya la taarab liitwalo 'Eagle Modern Taarab na tayari tumeshakamilisha nyimbo mbili kati ya tano tunazoandaa kwa ajili ya albamu yetu ya kwanza," alisema Hammer Q.
Nyota huyo aliyetamba na vibao kama Pembe la Ng'ombe na Kitu Mapenzi akiwa Dar Modern, alisema kundi lao lina wasanii 16 baadhi yao wakiwa ni wale aliokuwa nao kundi la Dar Modern kama Latifa Salum, Ramadhani Kisolo na Aisha Athuman.
Wengine wanaounda kundi hilo jipya lililokua wiki chache tangu kuanzishwa kwa kundi jingine la Tanzania Moto Taarab ni; Mwanaidi Ramadhani, Asma Ally, Mohammed Mzaka na wengineo waliopo kambini wakijiandaa na kujitambulisha rasmi kwa mashabiki wa miondoko hiyo.
Hammer Q, alisema tayari nyimbo tano za albamu yao zimekamilika na kuzitaja majina yake na waimbaji wake kuwa ni; 'Tatu Bila'-Hammer Q, 'Zangu Dua'-Latifa Salum, 'Kunyamaza Kwangu'- Mwanaidi Ramadhani, 'Siri ya Mungu'-Aisha Athuman na 'Mapenzi ya Dhati'-Asma.

No comments:

Post a Comment