Kocha wa zamani wa Simba, Milovan Cirkovic |
HATMA ya aliyekuwa kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic, kulipwa fidia yake ya kusitisha mkataba wa kuifundisha timu hiyo huenda ikajulikana leo wakati atakapokutana na viongozi wa klabu hiyo kabla ya kurejea kwao baada ya kupata haki yake.
Hata hivyo, Milovan ambaye ameumizwa na sare ambazo Simba imeendelea kuzipata, alisema jana kwamba yuko tayari kurejea kwenye timu hiyo endapo uongozi utamrejesha.
Milovan anaidai Simba dola za Marekani 24,000 (Sh. milioni 36), ambazo ni malimbikizo ya mishahara yake ya miezi mitatu.
Akizungumza jana, Milovan, alisema kwamba hadi sasa anafahamu kuwa yeye bado ni kocha halali wa timu hiyo kwani mkataba wake unamalizika Julai Mosi mwaka huu.
Mserbia huyo alisema kwamba ndiyo maana, baada ya kuona viongozi wa klabu hiyo wakikaa kimya, aliamua kuja nchini kufuatilia haki yake na kwamba, hata hoteli anayoishi jijini Dar es Salaam gharama zake zitalipwa na Simba.
"Mimi najua bado ni kocha wa Simba kwa sababu mkataba wangu haujamalizika. Na kama watakuwa tayari kuzungumza na mimi, naweza kurejea kazini. Bila shaka mnajua uwezo wangu na nini nilikifanya katika ligi na mshindano ya kimataifa mwaka jana," alisema kocha huyo.
Aliongeza kwamba kabla ya kukutana leo na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alitarajiwa kukutana jana na katibu mkuu wa timu hiyo, Evodius Mtawala; ambaye ndiye huwasiliana naye mara kwa mara.
"Hata hivyo, naye aliahidi tutakutana leo (jana) asubuhi, lakini sijamuona na alisema kwamba anamsubiri Rage na Kaburu," aliongeza Milovan.
Akihojiwa juzi katika kipindi cha michezo cha Radio One, Rage alikiri kocha huyo kuidai Simba lakini akashangazwa na maamuzi yake (Milovan) kufuata malipo yake jijini Dar es Salaam wakati wao walimueleza kuwa watamtumia kwa njia salama za kibenki.
Milovan alitua jijini Jumatano wiki iliyopita na kulieleza gazeti hili kwamba amechukua maamuzi ya kufuata haki yake baada ya kuona ahadi alizopewa kwa njia ya simu hazitekelezwi na kwamba sasa, anafahamu kuwa klabu hiyo inazo fedha baada ya kumuuza kwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia aliyekuwa mshambuliaji wao wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi.
CHANZO:NIPASHE
No comments:
Post a Comment