STRIKA
USILIKOSE
Friday, June 1, 2012
Malipo kiduchu yamkimbiza bondia ulingoni
BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Saleh Mkalekwa, amesema malipo madogo wanayolipwa mabondia wengi akiwemo yeye yamefanya wengi wao kufa maskini, jambo linalomfanya afikirie kuachana na mchezo huo kabla ya kutimiza ndoto zake.
Akizungumza na MICHARAZO
, Mkalekwa mwenye rekodi ya kucheza mara saba, akishinda sita na kupoteza moja, alisema alipotumbukia katika ngumi alikuwa na ndoto nyingi ikiwemo kutamba kimataifa, ila amekatishwa tamaa na malipo kiduchu anayolipwa.
Alisema hali ya kulipwa kidogo haipo kwake tu, bali karibu mabondia wote ambao licha ya kuhatarisha maisha yao wamekuwa hawathaminiwi zaidi ya kuwanufaisha wasimamizi wa mchezo huo wakiwemo mapromota.
Mkalekwa alisema kutokana na hali hiyo anafikiria kuachana na mchezo huo kwani haoni faida anayopata zaidi ya kuhatarisha maisha yake na kuwanufaisha waandaaji ambao wamekuwa wakiweka mbele masilahi yao kuliko ya mabondia na ngumi kwa ujumla.
"Kwa kweli nilitamani mno kufika mbali kama walivyofika wakali wengine, lakini kwa jinsi tunavyonyonywa na kutumiwa kuwaneemesha wengine, ngumi zimenitumbukia nyongo," alisema.
Alisema tangu alipoanza kupanda ulingoni mwaka 2008 hajawahi kulipwa pigano lolote malipo yanayozidi Sh 100,000, licha ya gharama kubwa za kuajiandaa na michezo hiyo kitu ambacho akihoji anaambiwa acheze kwanza ili akuze jina lake.
"Wenzetu katika soka, hata kama ni chipukizi, wanalipwa fedha ambazo zinawatia nguvu kuendelea kuufurahia mchezo huo sio sisi, ndio maana unaona nimejiweka kando nikijifanyia mazoezi mwenyewe nikishughulisha na biashara ya spea za magari," alisema.
Hata hivyo bondia huyo alisema iwapo atafanikiwa kupata mtu wa kumsaidia kumtafutia michezo yenye malipo ya kuridhisha na hasa ile ya kimataifa atakuwa tayari kuendelea na ngumi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment