Jacklyne Wolper na 'watoto wa Kanumba' |
Leah Richard 'Lamata' |
FILAMU mpya ya kumuenzi aliyekuwa nyota wa zamani wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba iitwayo 'After Death', inatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu msanii huyo alipofariki dunia Aprili 7.
Mmoja wa waratibu wa filamu hiyo, Leah Richard 'Lamata' alisema wameamua kuupeleka uzinduzi huo Aprili 7 mwakani, ili kuleta maana halisi ya kumuenzi nyota huyo aliyefariki ghafla nyumbani baada ya kutokea mzozo na mpenziwe.
Lamata, ambaye ndiye muongozaji wa filamu hiyo iliyotungwa na Jacklyne Wolper, alisema awali walipanga wafanye uzinduzi huo Februari, lakini wakaona isingeleta maana ilihali Kanumba alifariki mwezi Aprili na hivyo wamepeleka hadi tarehe hiyo.
"Uzinduzi wa filamu maalum ya kumuenzi Kanumba, iitwayo 'After Death' ambayo tulipanga kuizindua Februari sasa itazinduliwa Aprili 7, ambayo itakuwa siku ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu msanii huyo alipofariki," alisema Lamata.
Lamata mmoja wa waongozaji mahiri wa filamu nchini, alisema anaamini siku hiyo itawapa fursa nzuri mashabiki wa filamu hasa waliomzimia Kanumba kumuenzi na kushuhudia baadhi ya kazi za mkali huyo.
Alisema After Death, iliyoigizwa na karibu wasanii wote waliowahi kufanya kazi na Kanumba, itawarejeshea kumbukumbu mashabiki wa filamu kutokana na msanii Philemon Lutwaza 'Uncle D' kucheza nafasi ya nyota huyo aliyefanana naye.
Wengine walioshiriki filamu hiyo ni Mayasa Mrisho, Jacklyne Wolper, Patcho Mwamba, Ben Blanco, Irene Paul, Ruth Suka 'Mainda' na watoto walioibuliwa na marehemu Kanumba kupitia 'This is It' na 'Uncle JJ' Patrick na Jennifa.
No comments:
Post a Comment