STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 26, 2013

Suarez ruksa kuteta na Arsenal, ila...!

http://i.telegraph.co.uk/multimedia/archive/02489/luis-suarez_2489623b.jpg
LONDON, Uingereza
LUIS Suarez ataruhusiwa kufanya mazungumzo na Arsenal baada ya klabu hiyo ya London kufikisha ofa ya paundi milioni 40 lakini Liverpool haiko tayari kumuuza mshambuliaji huyo hadi bei ya paundi milioni 50 itakapofikiwa.
Ofa iliyoweka rekodi ya Arsenal ya paundi milioni 40 jumlisha paundi moja ilikataliwa na Liverpool lakini Suarez sasa anataka kufanya mazungumzo na klabu hiyo ya London.
Ripoti nyingine zinasema mshambuliaji huyo amewaambia maafisa wa Liverpool kwamba anataka kujiunga na Arsenal na anajiandaa kuwasilisha barua ya kuomba kuondoka Anfield.
Ofa ya paundi milioni 40 inamaanisha kwamba kipengele cha kuvunjia mkataba wake kimefikiwa na hivyo ni lazima Liverpool imfahamishe kuhusu ofa hiyo na sasa yuko huru kuzungumza na Arsenal.
Arsenal wanajiandaa kumlipa Suarez mshahara wa paundi 150,000 (Sh. milioni 364) kwa wiki kwa mkataba wa miaka mitano.
Lakini Liverpool haiko tayari kumuuza hadi Arsenal watakapoongeza ofa yao.
Juzi Jumatano, Suarez aliichezea Liverpool kwa mara ya kwanza tangu tukio maarufu la kumng'ata mkononi beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic msimu uliopita, akiingia kutokea benchi katika dakika 18 za mwisho za mechi yao ya kirafiki waliyoshinda 2-0 dhidi ya Melbourne Victory kwenye Uwanja wa MCG.
Huku Liverpool ikiongoza kwa goli 1-0, Suarez alipika goli la pili la timu hiyo wakati alipomtengea mchezaji mpya Iago Aspas katika dakika za lala salama.
Baada ya mechi hiyo kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers alisema: "Hakuna kipya cha kueleza, yeye (Suarez) ni mchezaji wa Liverpool na ndani ya wiki chache zijazo tunahitaji kumrejeshea kasi yake."
Rodgers hata hivyo, alimkumbusha Suarez deni alilonalo kwa mashabiki wa Liverpool ambao walisimama upande wake kwa misimu miwili ambayo ametawaliwa na matukio ya utata.
"Sapoti aliyopata kutoka kwa mashabiki na watu wa mji wa Liverpool haipimiki," Rodgers aliongeza.
"Katika kipindi hicho alikosa mechi nyingi za timu kutokana na sababu mbalimbali. Watu walisimama upande wake kama mtoto wao na hakika walikuwa wakimtetea. Chochote kitakachotokea katika wiki zijazo jambo hilo litabaki akilini mwake kwa sababu ni mambo ambayo huwezi kuyasahau."
Liverpool sasa wamekataa ofa mbili kutoka Arsenal, ambao wamedhamiria kuimarisha safu yao ya ushambuliaji, wakati Real Madrid, ambao tayari wamemuuza Gonzalo Higuain kwa Napoli, bado pia wanamhitaji nyota huyo wa Uruguay licha ya kwamba hawajapeleka ofa yoyote.
Kufuatia ofa mpya ya Arsenal, mmiliki wa Liverpool, John Henry aliwakebehi katika ukurasa wake wa Twitter kwa kuandika: "Unadhani wanavuta/puliza nini kule Emirates?"
Haijawa wazi kama kama Henry anazungumzia majaribio ya Arsenal kutaka kumsajili Suarez au kiasi cha ofa wanazotuma.
Wakati Liverpool wanadhamiria kumbakisha Suarez, ambaye alifunga magoli 30 katika mechi 44 za klabu hiyo msimu uliopita, ugumu wao unatarajiwa kulegea kama kama ofa hiyo itazidi kuongezwa. Kama ofa ya Arsenal itakubaliwa, itakuwa ni zaidi ya mara mbili ya kiwango cha juu cha pesa walichotoa kumnunua mchezaji.
Arsenal, ambao ofa yao ya kwanza kwa Suarez ilikuwa ni paundi milioni 30, walilipa paundi milioni 17.5 kumnunua winga wa Sevilla, Jose Antonio Reyes mwaka 2004.
Suarez anataka kuondoka Anfield ili akacheze soka la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya licha ya kwamba alisaini kurefusha mkataba wake Liverpool mwaka jana tu.
Uvumi ulianza kukua kuhusu hatma ya Suarez tangu alipofungiwa mechi 10 mwishoni mwa Aprili kwa kumng'ata Ivanovic.
Mshambuliaji huyo amebakisha mechi sita za kutumikia katika kifungo chake na pia alifungiwa mwaka 2011 baada ya kukutwa na hatia ya kumfanyia vitendo vya kibaguzi beki wa Manchester United, Patrice Evra.
Suarez alijiunga na Liverpool akitokea Ajax Januari 2011 kwa ada ya uhamisho ya paundi milioni 22.7.
Wachezaji walionunuliwa na Arsenal kwa pesa nyingi zaidi ni Jose Antonio Reyes (paundi milioni 17.5 kutoka Sevilla), Santi Cazorla (paundi milioni 16, Malaga), Andrey Arshavin (paundi milioni 15, Zenit St Petersburg), Sylvain Wiltord (paundi milioni 13, Bordeaux) na Thierry Henry (paundi milioni 11, Juventus).

No comments:

Post a Comment