STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, September 11, 2012

Hosea Mgohachi: Mpiga besi wa Extra afurahie muziki kumwezesha kimaisha

Hosea Mgohachi akiwa kwenye pozi kwenye ukumbi wa White House, Kimara

Moja ya nyumba za mwanamuziki Hosea Mgohachi
Hosea Mgohachi akicharaza gitaa kwenye mazoezi ya bendi yake ya Extra Bongo
Hosea akionyesha manjonjo yake kwenye moja ya maonyesho ya Extra Bongo nchini Finland hivi karibuni ilipoenda kwa ziara maalum nchi za Scandinavia
WAKATI wasanii na wanamuziki wengine wakilia kwamba fani zao zimekuwa zikishindwa kuwanufaisha kimaisha kwa sababu hizi na zile, kwa mkung'uta gitaa la besi wa Extra Bongo, Hosea Mgohachi 'Fukuafuku' kwake ni tofauti. Mgohachi, anasema anashukuru Mungu muziki aliouanza tangu akiwa kinda akiimba na kupiga ala shuleni na kanisa la Anglican-Kurasini, umemsaidia kwa mengi kiasi hajutii kujitosa kwke kuifanya fani hiyo. "Sio siri muziki umenisaidia mengi kiasi najivunia fani hii kwani, imeniwesha kumiliki nyumba mbili zilizopo Mbagala Kilungule na Mbagala Kuu, pia nina mradi wa 'Bodaboda' wenye pikipiki kadhaa," anasema. Mbali na hayo, Mgohachi anasema muziki umemwezesha pia kutembea nchi kadhaa duniani, kupata rafiki na kuitunza familia yake kwa pato la fani hiyo. Mgohachi, mwenye ndoto za kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa, anasema siri ya mafanikio yake imetokana na nidhamu yake katika matumizi ya fedha na kiu kubwa aliyonayo ya kuwa mfanyabiashara atakapostaafu muziki. "Mtu hupata mafanikiokwa kujituma kwa bidii, ila kubwa ni suala la nidhamu hasa kwa matumizi ya fedha, kitu ambacho nimekuwa nikizingatia kwa muda mrefu hadi kufika hapa nilipo," anasema. Anasema hata kwa wasanii na wanamuziki wenzake ni vema wakazingatia hilo iwapo wanataka kufika mbali licha ya ukweli pato litokanalo na sanaa kukiri kuwa dogo kulinganisha na ukubwa wa kazi. MDUDU Mpiga gitaa huyo aliyesoma darasa moja na nyota wa muziki wa kizazi kipya anayetamba kundi la Wanaume Halisi, Sir Juma Nature, anasema wakati akichipukia kwenye muziki alivutiwa na kwaya za St James na Kristo Mfalme. Ila kwa sasa anadai anakunwa na wapiga gitaa Minicha na Kapaya waliopo pamoja na nyota wa DR Congo, Werrason Ngiama Makanda na mpiga solo nyota wa Extra Bongo, aliyewahi kutamba na bendi kadhaa nchini Ephrem Joshua 'Kanyaga Twende'. "Hawa jamaa nawazimia sana kwa ucharazaji wao wa magitaa, hasa Joshua, yaani tukiwa kundi moja utashangaa vitu tunavyotoa," anasema. Mkali huyo, anayeitaja Extra Bongo kama bendi bomba kwake kwa namna inavyomtunza na kumlipa dau kubwa kuliko bendi zote alizowahi kuifanyia kazi, anasema hakuna chakula anachopenda kula nyama ya nguruwe maarufu kama 'Kitimoto' au 'Mdudu'. "Aisee katika vyakula ninavyopenda kula hakuna kama 'mdudu' yaani ukitaka kunifurahisha we nipe nyama hii kwa ndizi za kuchoma ," anasema. Mgohachi, ambaye hajaoa kwa sasa ingawa yu mbioni kufanya hivyo kwa mwanamke anayeishi naye, anasema pia anapenda kunywa soda na siku moja moja kusuuza roho yake kwa kugida bia. OKWI Akiwa na watoto watatu, Wilson, 7 anayesoma darasa la pili Shule ya Msingi Mwananyamala, Mery, 7, anayesoma darasa la pili Shule ya Msingi Mtoni na Junior, 3, Mgohachi anasema japo soka halicheza sana utotoni mwake, lakini ni shabiki mkubwa wa mchezo huo. Anasema yeye ni shabiki mkubwa wa Simba na Manchester United akimtaja Emmanuel Okwi anayichezea Simba kama anayemkuna kwa umahiri wake wa kufumania nyavu uwanjani. "Kati ya nyota wanaonipa raha katika soka Emmanuel Okwi ndiye kinara wao, huyu jamaa ana akili ya kufunga, mjanja na ana kipaji cha kipekee hata Yanga wanamjua," anasema kwa utani huku akicheka. Mgohachi anayepiga magitaa yote na kupapasa kinanda, anasema hakuna tukio la furaha maishani mwake kama alipomaliza kujenga nyumba yake ya Mbagala Kuu na kusitikishwa na kifo cha dada yake kilichotokea mwaka 1999. Juu ya muziki wa Tanzania, Mgohachi anayeiomba serikali iitupie macho fani ya sanaa ili kuwainua wasanii, anasema umepiga hatua kubwa tofauti na miaka ya nyuma, ingawa anataka wanamuziki kubadilika na kuwa wabunifu zaidi./ Anasema ubunifu utaweza kuutangaza muziki huo kimataifa kama ilivyokuwa ikifanywa na makundi kama Tatu Nane, InAfrica Band na wengine. "Lazima tuwe wabunifu tuweze kutamba kimataifa, tuachane na kasumba na kupenda kuwaiga wakongo tunawatangaza zaidi wao badala ya muziki wetu," anasema. ALIPOTOKA Hosea Simon Mgohachi, alizaliwa Aprili 14, 1978 jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa nne kati ya watano wa familia yao, alisoma Shule ya Msingi Kurasini alipoanza kuonyesha kipaji chake cha sanaa akiimba kwaya na kupiga ala. Mbali na shuleni, Mgohachi pia alikuwa akiimbia kwaya ya kanisa lao la Anglican chini ya walimu Charles na Yaredi Disanura kabla ya kupitia makundi ya Chikoike Sound na Mwenge Jazz. Bendi yake ya kwanza kuifanyia kazi kama mwanamuziki kamili ni African Beat mnamo mwaka 1998 kabla ya kutua Mchinga Sound 'Wana Kipepeo' akiwa na rafikie Ibrahim Kandaya 'Profesa' aliyepo Msondo Band kwa sasa. Bendi nyingine alizofanyia kazi mwanamuziki huyo anayewaasa wasanii wenzake na watanzania kwa ujumla kujiepusha na Ukimwi kwa kujenga utamaduni wa kuwa waaminifu na kupima afya zao sawia na kutumia kondomu inaposhikana ni Double M Sound, Double Extra, Chipolopolo na African Vibration. Pia amewahi kufanya kazi za muziki Umangani kwa zaidi ya mara mbili wakati akiipigia bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' kabla ya mwaka jana kuhamia Extra Bongo alionao mpaka sasa akiwa amerejea nao kutokea nchi za Skandinavia. Mgohachi anayependa kutumia muda wake kuangalia vipindi vya runinga na kusikiliza muziki wa Bongofleva akimzimia Sir Juma Nature anasema atakuwa mchoyo wa fadhila kama hatawashukuru wazazi wake, Mama Shuu, Mudhihir Mudhihir na Ally Choki kwa namna walivyomfikisha hapo alipo.

Hosea Mgohachi akiwa katika pozi
Hosea Mgohachi akiwa na mwanae Junior

No comments:

Post a Comment