FAINALI za kumtafuta bingwa wa kuhifadhi Q'uran kwa njia ya kughani (Tajuweed) mwaka huu zitafanyika kwenye Msikiti wa Manyema jijini Dar es Salaam, Ijumaa ya mwisho ya mfungo mtukufu wa Ramadhani Julai 25 mwezi huu.
Aidha, siku hiyo itakuwa ni sawa na funga ya 27 ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, hivyo waumini wa dini ya Kiislamu watakuwa ndani ya maombi maalum maarufu kama “Lailatul Qadir” ambayo huyatumia kuomba msamaha na kufutiwa madhambi maradufu na Mwenyezi Mungu.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Taasisi ya Kuhifadhi na Usomaji wa Kuran ya Sheikh Yahya Hussein (Sheikh Yahya Hussein Tahfidh Q’uran and Tajweed Foundation), Maalim Hassan Yahya katika taarifa aliyotuma kwenye vyombo vya habari mwishoni mwa wiki.
Maalim alisema fainali hizo zitawakutanisha washindi wote wa michuano ya kusoma Koran watakaokuwa wameshinda kwenye michuano ya taasisi mbalimbali inayoendelea hivi sasa Afrika Mashariki na Kati.
“Tutakuwa na washindanaji walioshinda kutoka nchi zote za Afrika Mashariki na Kati ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Congo DRC, Sudan Kusini na Tanzania,”alisema Maalim
Aidha alisema kuwa kutakuwa na majaji kutoka nchi hizo na wengine kutoka Saudi Arabia na Iran.
Alisema kuwa ni washindi watatu wa mwanzo watapata nafasi ya kwenda Hijjah kwa gharama za taasisi yake pia watazawadiwa vyeti na fedha taslimu.
No comments:
Post a Comment