LONDON, England
KOCHA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger
amemwagia sifa kiungo wa West Ham na ambaye wanamfukuzia kumnasa katika kipindi
hikicha usajili wa dirisha dogo la Januari, Mohamed Diame.
Arsenal wamekuwa wakihusishwa mara kwa
mara na usajili wa kiungo huyo mwenye miaka 25, anayeaminiwa kuwa na kipengele
katika mkataba wake kinachomruhusu kuondoka ikiwa zitalipwa paundi za England
milioni 3.5 (Sh. bilioni 9)
Diame ameonyesha kiwango cha juu na
kuibuka kuwa mmoja wa wachezaji nyota wa klabu hiyo msimu huu, akifunga mabao
mawili, yakiwamo dhidi ya Arsenal katika
mechi yake ya 18 tangu aanze kuichezea timu hiyo inayoongozwa na kocha Sam
Allardyce.
Wenger ameongeza uvumi kuhusiana na kiungo
huyo mwenye mwili 'jumba' wa timu ya taifa ya Senegal, akiwaambia waandishi wa
habari: "Anafanya vitu vikubwa katika mechi, nimemuona akionyesha kiwango
cha juu."
Arsenal ilifungwa 2-1 katika mechi yao
dhidi ya Chelsea Jumapili, hivyo kuambulia pointi moja tu katika mechi tatu
zilizopita za Ligi Kuu ya England ambazo zinawafanya waachwe kwa pointi saba na
mahasimu wao katika kuwania nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya
England, Tottenham na pia kulingana na Liverpool na West Brom ambao wote wana
pointi 34.
Hata hivyo, kuna habari njema kwa Arsenal
kufuatia taarifa za kupona kwa kiungo wao Mikel Arteta aliyekuwa nje kutokana
na majeraha.
No comments:
Post a Comment