STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 23, 2013

Azam yarejea nchini kamili gado

Kikosi cha Azam

MABINGWA wa Kombe la Mapinduzi, Azam Fc wanatarajiwa kurejea leo usiku Dar es Salaam, wakitokea Nairobi, Kenya walipokwenda kwa ziara ya wiki moja hya michezo ya kujipima nguvu kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
AZAM FC yenye maskani yake Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ilihitimisha vema ziara yake hiyo jana, baada ya kuifunga timu ya Benki ya Biashara Kenya, KCB bao 1-0 kwenye Uwanja wa City, Nairobi jioni hii.
Bao pekee la ushindi la Azam jioni ya jana lilifungwa na kiungo Ibrahim Mwaipopo kwa shuti la mpira wa adhabu katika dakika ya pili ya muda wa nyongeza, baada ya kutimu kwa dakika 45 za kawaida za kipindi cha kwanza.
Hata hivyo, Azam ingeweza kuondoka na ushindi mnene zaidi jana, kama si kiungo wake mwingine Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ kukosa penalti dakika ya 83 baada ya shuti lake la kudakwa na kipa wa KCB.
Huo unakuwa ushindi wa pili katika mechi zake tatu za kujipima nguvu nchini humo, kwani awali bao pekee la Gaudence Exavery Mwaikimba kwa penalti dakika ya 58 liliipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Sofapaka ya Kenya kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Katika mchezo wake wa kwanza, mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi walifungwa mabao 2-1 na AFC Leopard kwenye Uwanja huo huo wa Nyayo.
Pamoja na kufungwa na Leopard, Azam watajilaumu wenyewe, kwani walipoteza penalti mbili kupitia kwa Joackins Atudo na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Mabao ya Leopard katika mchezo huo, yalifungwa na Paul Were na Mike Barasa, wakati la Azam lilifungwa na Sammih Hajji Nuhu kwa penalti.
Azam ilimaliza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi zake 24, nyuma ya vinara Yanga waliomaliza na pointi 29, wakati Simba walimaliza nafasi ya tatu kwa pointi zao 23.
Pamoja na Ligi Kuu, Azam pia itacheza Kombe la Shirikisho la Soka Afrika na itaanza na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini mjini Dar es Salaam kati ya Februari 15 na 17 mwaka huu.
Mechi hiyo itachezeshwa na marefa wa Kenya, katikati Davies Omweno na atakayesaidiwa na mwamuzi msaidizi namba moja Peter Keireini, mwamuzi msaidizi namba mbili Gilbert Cheruiyot wakati mwamuzi wa mezani Anthony Ogwayo.
Kamisaa wa mechi hiyo atakuwa Hassan Mohamed Mohamud kutoka Somalia, wakati marefa wa mechi ya marudiano itakayochezwa mjini Juba wiki mbili baada ya mechi ya kwanza watatoka Rwanda, wakiongozwa na Gervais Munyanziza.


CHANZO:BIN ZUBEIRY

No comments:

Post a Comment