Msanii Baby J |
Baby J, alisema ubinifu na kulinda mila na asili ya kitanzania inaweza kuwa njia rahisi ya kujitambulisha kimataifa kuliko tabia ya kuiga kazi za watu na tamaduni za kigeni.
Akizungumza na MICHARAZO katika mahojiano maalum, msanii huyo anayetoka visiwani Zanzibar, Baby J alisema tabia ya kuiga kazi za wasanii wa nje au kuuiga utamaduni wa wa kigeni unawafanya wasanii wa Tanzania kushindwa kujitangaza kimataifa.
Baby J, alisema ni vema wasanii wakaumiza vichwa vyao kubuni vitu vyao wenyewe pamoja na kuhakikisha katika kazi zao zinaegemea katika mila na tamaduni za kitanzania ili hata zikishindanishwa nje ya nchi iwe rahisi kutambulika kuliko ilivyo sasa.
"Kwa kuwa muziki wetu umepiga hatua kubwa kwa sasa kulinganisha na siku za nyuma ni vema sasa wasanii wakabadilika na kubuni kazi zao wenyewe wakizingatia mila na asili ya Tanzania ili kujitambulisha kwa urahisi kimataifa," alisema.
Kuhusu mipango yake, Baby J, alisema kwa sasa yu mbioni kuachia hadharani wimbo wake wa nane uitwao 'Nimempenda Mwenyewe' aliomshirikisha Diamond.
"Wimbo umeshakamilika na utakuwa wimbo wangu wa nane baada ya awali kutoa nyimbo saba nilizoshirikisha wasanii kadhaa nyota kama Chid Benz, Pasha, Ally Kiba na Banana Zorro na wengine," alisema Baby J.
Msanii huyo ambaye ni mke wa mtu alianza kufahamika kwenye ulimwengu wa muziki mwaka 2006 alipotoka na wimbo uitwao 'Mpenzi wa Moyo' alioimba na Taqwa.
No comments:
Post a Comment