STRIKA
USILIKOSE
Tuesday, January 21, 2014
Uganda yakwama CHAN, tumaini la CECAF lipo kwa Burundi sasa
WAWAKILISHI wa CECAFA katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) inayoendelea Afrika Kusini, Uganda The Cranes usiku wa kuamkia leo imejikuta ikikwama kusonga mbele kwa kulala 3-1 kwa Morocco.
Uganda waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kutamba kwenye kundi lake, imejikuta ikiaga mashindano hayo kutokana na Zimbabwe kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Burkina Faso na kuifanya ifungane pointi tano sawa na Morocco na kufuzu.
The Cranes wamesalia na pointi zao nne na Morocco wamemaliza kama vinara wa kundi hilo wakifuatiwa na Zimbabwe.
Katika pambano hilo la Uganda na Morocco washindi walianza kupata bao la kwanza lililozamishw na Rafik Abdessamad katika dakika ya 29 akimaliza kazi nzuri ya Abdelkabir El Ouadi, bao lililodumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa Uganda kurejesha bao hiulo kupitia mfungaji wake nyota, Yunus Sentamu katika dakika ya 60 kabla ya Nouhssine Iajour kuiongezea Morocco bao la pili dakika ya 77 na El Ouadi kupigilia msumari wa mwisho kwa kufunga bao la tatu kwenye dakika ya 90'+3.
Katika pambano jingine lililochezwa kwa wakati mmoja sawa na pambano hilo la Uganda na Morocco, goli pekee la Zimbabwe lilitupiwa kimiani na Masimba Mambare katika ya 56 akimalimalizia kazi ya Kudakwashe Mahachi.
Morocco na Zimbabwe zimeunga na timu za Nigeria na Mali katika hatua ya robo fainali, huku washindi wengine wakitarajiwa kupatikana leo baada ya mechi za kundi C ambapo Ethiopia iliyokwisha yaaga mashindano hayo mapema itavaana na Ghana na Jamhuri ya Kongo kupepetana na Libya.
Mpaka sasa kundi hilo linaongozwa na Libya yenye pointi nne sawa na Ghana ila zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, kisha kufuatia Kongo yenye pointi 3.
Mechi nyiungine za mwisho za makundi zitakazokamilisha idadi ya timu nane za kucheza hatua hiyo ya mtoano zitachezwa kesho kwa michezo kati ya Burundi dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Mauritania itakayoumana na Gabon.
Tumaini pekee la Ukanda wa CECAFA katika michuano hiyo imesalia mikononi mwa Burundi wanaoongoza kundi D ambapo italazimika kushinda kesho la sivyo ukanda huo utakuwa umepata aibu kwa timu zake zote tatu kuambulia patupu katika mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya tatu sasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment