Simba na Azam katika mechi yao ya Ligi Kuu duru lililopita |
Na Mwinyi Sadallah, Zanzibar
MABINGWA
watetezi wa Kombe la Mapinduzi, klabu ya Azam wanashuka dimbani kucheza
dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba katika mechi yao ya nusu
fainali ya Kombe la Mapinduzi 2012 kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar leo.
Mechi hiyo itaanza saa 2:00 usiku, ikitanguliwa
na nusu fainali nyingine itakayochezwa jioni kati ya mabingwa wa Ligi Kuu ya
Kenya, Tusker na Miembeni ya mjini visiwani hapa.
Tusker wamefanikiwa kuingia fainali
wakiwa na pointi 7 na kuongoza katika kundi lao la A baada ya kushinda pia
katika mechi yao ya mwisho kwa bao 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Pemba.
Simba ambao wamekuwa wakionyesha kiwango
kizuri kadri mashindano hayo yanavyosonga mbele, walitinga nusu fainali wakiwa
pointi tano baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi
dhidi ya Bandari.
Azam pia waliingia hatua ya leo wakiwa na
pointi tano baada ya juzi kutoka sare na Mtibwa Sugar na hivyo kuongoza katika
kundi lao la B, huku Miembeni wakiingia nusu fainali wakiwa na pointi nne baada
ya kutoka sare ya 0-0 na Coastal Union ya Tanga.
Kocha wa Simba, Jamhuri Kihwelu alisema
kwamba lengo la timu yake ni kutwaa ubingwa baada ya wachezaji wake kuonyesha
kiwango kizuri tangu kuanza kwa mashindano hayo.
“Nia tunayo na uwezo wa kutwaa Kombe la
Mapinduzi mwaka huu tunao… wachezaji
wetu wameonyesha kiwango kizuri na hivyo naamini kesho (leo) tutashinda tu,”
alisema Kihwelu.
Kocha wa Tusker, Robert Matano, alisema
kwamba pamoja na timu yake kushiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo,
wachezaji wake wameonyesha kiwango kizuri na kufanikiwa kuongoza katika kundi
A, hivyo ni imani yake kwamba watashinda pia leo na kutinga fainali.
Hata hivyo, alisema kwamba timu zote
zilizofanikiwa kuingia nusu fainali ni nzuri na mafanikio yao yatatokana na
juhudi na maarifa ya wachezaji watakocheza leo.
Katibu wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi,
Abdallah Said, alisema bingwa wa mashindano ya mwaka huu atazawadiwa Sh.
milioni 10, mshindi wa pili Sh. milioni tano na mfungaji bora atazawadiwa Sh.
300,000.
Aliongeza kuwa mwamuzi bora wa mashindano
hayo na mwanahabari bora pia watapata zawadi ya Sh. 200,000 kila mmoja.
Fainali ya mashindano hayo zitafanyika
Jumamosi ambayo ni siku ya kilele cha maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar na
utachezwa pia kwenye Uwanja wa Amaan na kuhudhuriwa na mgeni rasmi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi.
CHANZO:NIPASHE
No comments:
Post a Comment