Ngassa na Bocco wakipongezana |
WASHAMBULIAJI Mrisho Ngassa wa Simba na
John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam ni miongoni mwa nyota zaidi walioripoti katika
kambi ya timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itakayosafiri leo jioni kwenda jijini Addis Ababa, Ethiopia kucheza
mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya wenyeji keshokutwa Ijumaa.
Awali, Bocco, Ngassa, kipa Juma Kaseja na
wachezaji wengine kadhaa walioitwa Stars kutoka katika klabu za Simba na Azam
walishindwa kuripoti katika kambi ya timu hiyo kwavile walikuwa na klabu zao
kwenye michuano inayoendelea visiwani Zanzibar ya Kombe la Mapinduzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface
Wambura, alisema kuwa nyota kutoka Simba, Azam na Mtibwa wameungana na wenzao
na kwamba sasa Stars itasafiri leo ikiwa na kikosi chenye wachezaji wengi zaidi
miongoni mwa wale walioutwa na kocha wao Mdenmark, Kim Poulsen.
Mbali na Bocco, Ngassa na Kaseja,
wachezaji wengine walioitwa Stars kutoka Simba, Azam na Mtibwa ni Shomari
Kapombe, Amri Kiemba, Amir Maftaha, Mwinyi Kazimoto, Salum Aboubakar 'Sure
Boy', Mwadini Ali, Mcha Khamis, Aggrey Morris,
Erasto Nyoni, Aishi Manula na nyota Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Shabani
Nditi kutoka Mtibwa Sugar,
"Stars inaondoka leo huku ikiwa
kamili baada ya nyota wengi kuripoti kambini," alisema Wambura.
Alisema timu hiyo itarejea jijini Dar es
Salaam baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Ethiopia na kuendelea na kambi
yao kujiandaa kwa mechi nyingine mbili za kirafiki, zote zikiwa ni sehemu ya
maandalizi kabla ya mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la
Dunia dhidi ya Morocco itakayochezwa Machi.
No comments:
Post a Comment