STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, February 26, 2014

Symbion kusaidia programu za vijana za TFF


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Symbion Power Tanzania Limited zimesaini makubaliano ambapo kampuni hiyo itasaidia kwenye maeneo matatu ya mpira wa miguu wa vijana.
Makubaliano hayo yametiwa saini leo (Februari 26 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam. Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesaini kwa niaba ya shirikisho wakati upande wa Symbion aliyesaini ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Peter Gathercoles.
Maeneo ambayo Symbion itasaidia ni ujenzi wa vituo viwili vya kuendeleza vipaji vitakavyojengwa Kidongo Chekundu na Kinondoni mkoani Dar es Salaam, mashindano ya Taifa ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 12 (U12) yatakayofanyika mwaka huu na kuisaidia timu ya U17 ya Tanzania (Serengeti Boys).
Serengeti Boys itacheza na Afrika Kusini, Julai mwaka huu katika mechi za mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa wachezaji wa umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Niger.
Hivyo Symbion imetoa dola 60,000 (zaidi ya sh. milioni 96) kwa ajili ya mashindano ya U12, na dola 50,000 (zaidi ya sh. milioni 80) kwa ajili ya maandalizi ya Serengeti Boys kwa mechi dhidi ya Afrika Kusini.
Rais Malinzi ameishukuru Symbion kwa kukubali kushirikiana na TFF katika mpira wa miguu wa vijana, lakini vilevile amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete kwani ndiye chachu ya kampuni hiyo kuamua kujishirikisha na mpira wa miguu wa vijana.

No comments:

Post a Comment