MWANAMUZIKI Mkongwe wa muziki wa dansi, Abuu Semhando 'Baba Diana', 57, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajili ya barabarani anatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda wilayani Muheza, Tanga kuzikwa.
Kwa mujibu Meneja Masoko wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' aliyokuwa akiifanyia kazi marehemu huyo,Martin Sospeter ni kwamba Semhando aliyefahamika pia kama Lukasa enzi akiwa Super Matimila, atazikwa kesho nyumbani kwao Tanga, ingawa msiba upo Mwananyamala Kisiwani alipokuwa akiishi enzi za uhai wake.
Sospeter, alisema mwili wa marehemu kwa sasa upo Muhimbili na wanafanya mipango ya kuusafirisha kwenda kuzikwa kwao Tanga kesho alasiri.
"Marehemu anatarajiwa kusafirishwa kwao Tanga kwa ajili ya mazishi, ingawa kwa sasa msiba upo nyumbani kwake, Mwananyamala Kisiwani na mwili wake umeshapelekwa hospitali ya Muhimbili," alisema Sospter.
Meneja huyo alisema kuwa marehemu aliyezaliwa Oktoba 24, 1953 na kuanza muziki mwaka 1974 katika bendi ya Sola Tv kabla ya kupita bendi mbalimbali Twanga Pepeta aliyoiongoza kama Katibu wake, amewaachia pengo kubwa lisilozibika aslan.
"Ni pigo kwetu na tumeshtushwa na kuhuzunishwa na kifo chake cha ghafla," alisema Sospeter.
Kifo cha mkongwe huyo aliuyewahi kuzipigia bendi za Super matimila, Orchestra Toma Toma, Tango Musica, Diamond Sound 'Wana Kibinda Nkoy', Beta Musica kabla ya kuasisi Twanga Pepeta, kimekuja masaa machache tangu fani ya muziki kumpoteza Ramadhan MToro Ongalla aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Dk Remmy alifariki Jumatatu na kuzikwa Alhamis, huku Semhando na wanamuziki wenzake wakishiriki mwanzo mwisho katika msiba huo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment