STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, August 4, 2014

Stars si Riziki AFCON, kama kawa yanyukwa na Msumbiji

http://shaffihdauda.com/wp-content/uploads/2014/07/taifa.jpgUTEJA wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) mbele ya Msumbiji umeendelea baada ya kutolewa katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa wenyeji Msumbiji (Mambas) katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Zimpeto mjini Maputo.
Kwa ushindi huo, Mambas wamesonga mbele katika mashindano hayo kwa kutinga hatua ya makundi baada ya ushindi wa jumla wa mabao 4-3 baada ya awali kutoka sare ya 2-2 katika mechi iliyochezwa Julai 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mambas walimaliza kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Josemar sekunde chache kabla timu hizo hazijaenda mapumziko.
Mshambuliaji wa Taifa Stars na klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Samata, aliisawazishia timu yake bao la kwanza katika dakika ya 77 na kuufanya mchezo huo uzidi kuwa mgumu kwa pande zote mbili.
Dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho kupulizwa na mwamuzi, Dennis Batte kutoka Uganda, Domingues alizima ndoto za Taifa Stars kutinga hatua ya makundi baada ya kuipatia Mambas bao la pili na la ushindi.
Stars ilikuwa hivi; Deogratius Munishi ‘Dida’, Said Mourad, Shomary Kapombe, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Erasto Nyoni, Thomas Ulimwengu, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Mbwana Samata na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Katika benchi waliwapo Aishi Manula, Aggrey Morris, Oscar Joshua, Haroun Chanongo, Mrisho Ngassa, Simon Msuva na Amri Kiemba.
Baada ya kushindwa kutinga hatua ya makundi, Tanzania ikiwa chini ya kocha huyo, Mholanzi Mart Nooij, itasubiri kucheza mashindano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki huku ikiwa watazamaji kwenye fainali zijazo za Afcon zitakazochezwa nchini Morocco mwakani.
Wakati huo huo mjini Kigali juzi timu ya soka ya Taifa ya Rwanda (Amavubi) juzi Jumamosi ilifanikiwa kusonga mbele katika mashindano hayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuiondoa Congo kwa njia ya penalti 4-3 baada ya matokeo ya jumla kuwa 4-4.
Amavubi juzi ilipata ushindi wa mabao 2-0 ikiwa nyumbani wakati Congo nayo ilipata ushindi wa aina hiyo ilipokuwa nyumbani na kusababisha mechi hiyo kutinga hatua ya matuta.
Nyota wa mechi ya juzi mjini Kigali alikuwa ni kipa wa Amavubi, Jean Luc ‘Bakame’ Ndayishimiye, ambaye alidaka penalti tatu za Congo zilizopigwa na Ferebory Dore, Mael Francis Lepicier na Herman Lakolop wakati Delvin Chansel Ndinga, Silver Mbousi Ganvoula na Thierry Koulossa Bifouma walifunga.
Kwa upande wa Amavubi waliopata ni Jimmy Mbaraga, James Tubane, Emery Bayisenge na Patrick Sibomana wakati Haruna Niyonzima aligongesha mwamba na ile ya Meddy Kagere ilidakwa na kipa wa Congo, Chasel Mohikola Massa.
Amavubi sasa itaungana na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Nigeria, Afrika Kusini na Sudan kwenye Kundi A.
Harambee Stars ya Kenya jana ikiwa nyumbani ililazimishwa suluhu na Lesotho hivyo kuyaaga mashindano hayo kufuatia kichapo cha bao 1-0 ilichopata ugenini wiki mbili zilizopita.

No comments:

Post a Comment