STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, April 11, 2013

Messi aivusha Barca nusu fainali, Juve wakiona cha moto nyumbani

 
Pedro akishangilia bao lake la kusawazisha dhidi ya PSG jana usiku

NYOTA wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi usiku wa kuamkia leo alionyesha ni namna gani alivyo chachu ya mafanikio ya timu yake baada ya kuiwezesha Barcelona kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Messi aliyeingia kipindi cha pili wakati wenyeji Barca wakiwa nyuma kwa bao 1-0, alibadilisha taswira nzima ya mchezo huo uliochezwa uwanja wa Camp Nou na kuipa timu yake sare ya bao 1-1 dhidi ya wageni PSG ya Ufaransa.

PSG walitangulia kupata bao kupitia Javier Pastore na kuwapa wakati mgumu wenyeji waliokuwa wameelemewa licha ya  Xavi Hernendez kuweka rekodi ya kupiga pasi sahihi kwa asilimia 100 katika pambano hilo.

Mara baada ya kuingia uwanjani Messi aliifanya PSG kupoteza mwelekeo na yeye kutumia nafasi hiyo kutoa pasi murua kwa David Villa ambaye alimpasia Pedro aliyefunga bao la kusawazisha dakika ya 71.

Hata hivyo Barca wamefanikiwa kufuzu kwa sheria ya bao la ugenini baada ya kupata sare ya mabao 2-2 ugenini wiki iliyopita na hivyo kufanya matokeo ya jumla kuwa mabao 3-3 na kuiondosha PSG kwenye michuano hiyo.

Katika pambano jingine ambalo lilichezwa mjini Turin, Italia wenyeji na vinara wa ligi kuu ya Seria A, Juventus walishindwa kutamba nyumbani baada ya kunyukwa mabao 2-0 na Bayern Munich ya Ujerumani.

Ushindi huo wa Munich umeifanya timu hiyo kufuzu nusu fainali ikiungana na timu za Real Madrid, Borussia Dortmund na Barcelona kwa jumla ya mabao 4-0.

Katika mechi yao iliyopita iliyochezwa nchini Ujerumani, Juve walilala kwa mabao 2-0.

Bayern ilipata ushindi huo ugenini kupitia mabao yaMario Mandzukic aliyefunga katika dakika ya 64 akimalizia mpira wa faulo uliopigwa na kiungo Bastian Schweinsteiger kabla ya Claudio Pizarro kufuinga bao la pili dakika ya 90.

Hatma ya timu zipi zitakazokutana katika hatua hiyo inatarajiwa kufahamika kesho Ijumaa itakapotangazwa droo ndogo huku kukiwa na hofu Wahispania na Wajerumani waliofuzu hatua hiyo kukutana wenyewe kwa wenyewe.


No comments:

Post a Comment