STRIKA
USILIKOSE
Thursday, June 7, 2012
Madega awaonya Yanga kuhusu uchaguzi
WANACHAMA wa klabu ya soka ya Yanga wameonywa na kutakiwa kuwa makini katika uchaguzi wao mdogo utakaofanyika Julai 15, kwa kuhakikisha wanachagua viongozi wenye uchungu na nia ya dhati ya kuipeleka mbele klabu hiyo.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Imani Madega ambapo alisema uchaguzi huo unapaswa kutumiwa vema na wanachama wa Yanga kuhakikisha wanachagua viongozi wenye sifa na wataoikwamua klabu yao.
Madega, alisema pupa yoyote watakayofanya wanachama hao kwa kuchagua viongozi wasiokuwa makini maana yake ni kuiweka pabaya Yanga na huenda watu wakaanza kunyoosheana vidole kama ilivyotokea katika uongozi uliopita.
Mwenyekiti huyo wa zamani aliyeondoka madarakani kwa heshima kubwa ikiwemo kuiachia klabu hiyo akaunti iliyokuwa na fedha za kutosha, alisema ingawa katika kipindi kama hiki wanachama hunufaika, lakini waikumbuke klabu yao.
"Ni vema wanayanga wakawa makini katika uchaguzi huu kwa kuhakikisha wanachangua watu wa mpira, wenye upeo na uwezo wa kuiongoza Yanga ili itoke mahali ilipo na kuweza kuwa klabu yenye hadhi kimtaifa," alisema.
Kauli ya Madega imekuja wakati mchakato wa uchaguzi huo wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na waliokuwa viongozi wa Yanga, ambapo wagombea 28 kati ya 33 walirudisha fomu za kuwania uongozi katika kinyang'anyiro hicho.
Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi wa Yanga, Francis Kaswahili waliojitokeza kuwania nafasi ya Uenyekiti ni wagombea wanne ambao ni pamoja na Sarah Ramadhan, Edger Chibura na John Jambele.
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti pia ina wagombea wanne ambao ni meneja wa zamani wa klabu hiyo, Ayoub Nyenzi, Ali Mayay, Yono Kevela na Clement Sanga huku kwenye Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ina wagombea 20.
Wagombea hao ni nyota wa zamani wa timu hiyo akiwemo aliyekuwa nahodha Shaaban Katwila, Aaron Nyanda, Edger Fongo na Ramadhan Kampira.
Wengine wanaowania nafasi nne za ujumbe huo wa kamati ya utendaji ni Lameck Nyambaya, Mohammed Mbaraka, Ramadhani Saidi, Beda Tindwa, Ahmed Gao, Mussa Katabalo, George Manyama, Omary Ndula na Jumanne Mwamwenya.
Wagombea wengine ni Abdallah 'Binkleb' Mbaraka, Peter Haule, Justine Baruti, Abdallah Sheria, Jamal Kisongo, Gaudecius Ishengoma na Yona Kevela.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment