STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, June 7, 2012

Mchumiatumbo atamba hana mpinzani Bongo

BONDIA wa ngumi za kulipwa wa uzito wa juu, Alphonce Joseph 'Mchumiatumbo' ametamba kuwa, haoni bondia wa kupigana nae nchini kutokana na karibu mabondia wote wa uzito wake kuwachapa na wengine kuingia mitini kukacha kupigana nae. Aidha, amewaomba mapromota na wafadhili wa ngumi nchini kumsaidia kumtafutia mapambano ya kimataifa na mabondia wa nje ili awe kutimiza ndoto za kutwaa na kulitangaza jina lake katika anga hizo. Akizungumza na MICHARAZO kwenye mahojiano maalum, Mchumiatumbo alisema kutokana na kuwapiga karibu mabondia wote wa uzani wake na wengine kumkacha ulingoni anahisi hana bondia wa kupigana nchini hivyo kuwataka mabondia wa nje. Bondia huyo aliyepigana mapambano sita na kushinda matano, manne kati ya haayo kwa KO na kupata sare moja dhidi ya Ashraf Suleiman, alisema bondia aliyekuwa akidhani angeweza kumpa upinzani Amur Zungu alishaawahi kumkacha ulingoni. "Kwa kweli kama kila bondia ninayepigana nae naamshinda na wengine kunikacha ulingoni, sidhani kama kuna wa kupigana nami kwa sasa, hivyo nilikuwa naomba nitafutiwe michezo ya kimataifa kujitangaza zaidi na kuwania mikanda," alisema. Bingwa huyo wa zamani wa Mkoa wa Dar es Salaam wa ngumi za ridhaa, alisema mabondia wengi wa Tanzania wanaishia kutamba nchini tu kwa vile mapromota na waandaaji wa michezo ya ngumi hawawatafutii michezo ya kimataifa kama nchi nyingine. Mara ya mwisho Mchumiatumbo kupata ushindi ni wiki mbili zilizopita alipomtwanga kwa KO Bahati Mwafyale katika pambano lililofanyika kwenye ukumbi wa DDC Keko.

No comments:

Post a Comment