Haruna Niyonzima dimbani |
Na Sanula Athanas, Tanga
WACHEZAJI watatu wa Yanga akiwamo kiungo wao wa
kimataifa Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, waliumia vibaya katika mechi
yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya ‘maafande’ wa Mgambo JKT
iliyomalizika kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa juzi, imefahamika.
Akizungumza na NIPASHE wakati wa mazoezi ya Yanga
kwenye uwanja huo jana asubuhi, Daktari wa timu hiyo, Nassoro Matuzya alisema
kuwa Niyonzima aliumia vibaya pua yake alipogongana na beki 'kisiki' wa Mgambo,
Bashiru Chanacha dakika 12 kabla ya mechi hiyo kumalizika.
Matuzya, ambaye pia aliwahi kuwa daktari wa timu ya
taifa ya vijana (Serengeti Boys), alisema kuwa kugongana kwa wawili hao
kulisababisha kupasuka kwa jipu dogo alilokuwa nalo nyota huyo puani kwake.
Mwandishi alishuhudia pua ya Niyonzima aliyekuwa
amekaa kwenye benchi wakati wachezaji wengine wa Yanga wakiendelea na mazoezi
jana, ikiwa ‘imebomoka’ sehemu ya juu na baadhi ya nyama zikining’inia kwa
chini ndani ya matundu ya pua.
Hata hivyo, maofisa wa Yanga waliokuwa uwanjani
waliwakataza waandishi kumpiga picha kwa sababu jeraha alilokuwa nalo lilikuwa
linatisha.
Akizungumza kwa tabu, Niyonzima aliliambia gazeti
hili kuwa alikuwa akijisikia maumivu makali usiku wa kuamkia jana, lakini
anaamini kidonda hicho kitapona haraka ili arejee uwanjani kupambana kuwania
ubingwa wa 23 wa ‘Wanajangwani’.
“Kwa kweli mechi ya jana (juzi) ilikuwa ngumu.
Wapinzani (Mgambo) walikuwa wameikamia, walikuwa wanacheza rafu za kutisha.
Angalia pua yangu ilivyo. Usiku nimehangaika sana kupata usingizi. Kinachouma
zaidi marefa hawakutoa adhabu yoyote licha ya kufanyiwa faulo mbaya kama hii,”
alisema Niyonzima huku akishika pua yake.
“Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kupata pointi moja
kwa sababu tulicheza katika uwanja usiokuwa na hadhi na waamuzi hawakutenda
haki kwetu kwa kiasi kikubwa,” aliongeza mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya
maafande wa APR ya Rwanda.
Mbali na Niyonzima, ambaye mkataba wake na Yanga
unamalizika mwishoni mwa msimu huu, kiungo Frank Domayo na mshambuliaji Mganda
Hamis Kiiza pia wanasumbuliwa na majeraha baada ya kuumia katika mechi ya juzi.
Kwa mujibu wa daktari wa Yanga (Mtuzya), Kiiza ambaye
alishindwa kufanya mazoezi ya jana, aliumia kifundo cha mguu wa kulia dakika
moja kabla ya mapumziko ya mechi yao ya juzi na nafasi yake kuchukuliwa na mfungaji
bora wa Kombe la Kagame mwaka jana, Said Bahanunzi.
“Kiiza ameshindwa kufanya mazoezi kwa sababu jana
(juzi) aliumia kifundo cha mguu. Domayo nililazimika kumshona nyuzi mbili usoni
baada ya kupasuka,” alisema Matuzya.
Yanga waliondoka jijini hapa jana saa 5:24 asubuhi
kurejea Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi yao ya 24 ya ligi msimu huu dhidi ya
JKT Ruvu itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini humo.
Kabla ya kuondoka jijini hapa jana, meneja wa timu
hiyo, Hafidh Saleh alisema kuwa baada ya kutua Dar es Salaam, wachezaji
watapewa mapumziko ya saa 12 kabla ya kuingia tena kambini jijini humo
kujiandaa kwa mechi dhidi ya JKT Ruvu.
Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati Yanga wanaongoza
msimamo wa ligi ya Bara wakiwa na pointi 53, sita juu ya mabingwa wa Kombe la
Mapinduzi, Azam wanaokamata nafasi ya pili. Yanga wanahitaji pointi nne tu
kutawazwa mabingwa pasipo kujali matokeo ya Azam katika mechi tatu zilizobaki.
CHANZO:NIPASHE
No comments:
Post a Comment