Na Somoe Ng'itu
KATIKA kuhakikisha mwakani inakuwa na ukuta imara,
klabu ya Azam imeanza mikakati ya kumnasa beki tegemeo wa Simba na timu ya soka
ya Tanzania (Taifa Stars), Shomary Kapombe na tayari imetenga kiasi cha Sh.
milioni 60.
Mbali na kiasi hicho cha fedha pia Azam imepanga
kumpatia beki huyo kiraka gari jipya la thamani ya Sh. milioni 30.
Azam inataka kutumia udhaifu wa Simba kushindwa
kumpatia mkataba mpya beki huyo ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika
Desemba, jambo linalomaanisha anaweza kuondoka bure iwapo atakataa kusaini
mkataba mpya Msimbazi na pesa zote kutoka katika klabu itakayomsajili zitaingia
mifukoni mwake.
Hata hivyo, beki huyo amemweleza rafiki yake wa
karibu kwamba kiasi hicho ni kidogo kwa kiwango alichonacho hivi sasa.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini Dar es
Salaam, uongozi wa Azam, timu pekee nchini ambayo kwa sasa inashiriki
mashindano ya kimataifa, imetenga kiasi cha Sh. milioni tatu kama mshahara wa
kila mwezi wa beki huyo aliyesajiliwa na Simba akitokea timu ya Polisi Morogoro.
Chanzo kililiambia gazeti hili kuwa Azam wakifanikiwa
kumpata Kapombe, mikakati yao itakuwa ni kwa chipukizi Haruna Chanongo na
Ndembla Ibrahim.
"Wameanza maandalizi ya kumshawishi asisaini
mkataba mwingine wa Simba na wao watamsainisha ifikapo mwezi Agosti mwaka
huu," kilisema chanzo hicho.
Kapombe alishindwa kusema lolote kuhusiana na kuwapo
kwa mazungumzo dhidi ya Azam na kuongeza kwamba yeye kwa sasa ni mchezaji wa
Simba hivyo anajipanga kuisaidia timu yake ifanye vizuri katika mechi
zilizosalia.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, Kapombe ni
mmoja wa wachezaji mihimili wa klabu hiyo na hawatakuwa tayari kuona
wanasajiliwa na klabu nyingine.
Mtawala alisema kwamba Kapombe ni mchezaji muelewa na
kamwe hataweza kukurupuka na kukubali kuiacha Simba iliyomchukua hali ya kuwa
klabu yake imeshuka daraja.
"Anafahamu ana kiwango cha kucheza soka Ulaya na
Simba ni sehemu pekee inayoweza kutimiza ndoto zake, tutakaa naye na kumpa
mkataba mnono ndani ya muda muafaka," alisema katibu huyo mwenye taaluma
ya sheria.
Viongozi wa Azam, katibu mkuu Nassor Idrissa na
meneja Patrick Kahemele, hawakupatikana jana katika simu zao za mikononi
kuzungumzia mipango hiyo ya kumnasa Kapombe.
Hata hivyo, Azam imekuwa na kawaida ya kufanya
usajili wake kimya kimya na hutangaza mchezaji mpya baada ya kukamilisha
taratibu zote zinazotakiwa iwe kwa mchezaji wa ndani au nje ya nchi.
Chanzo:NIPASHE
No comments:
Post a Comment