MBIVU na mbichi ya nani mkali katika fani ya filamu kwa mwaka 2012 zinatarajiwa kufahamika mwezi ujao wakati wa hafla ya kutangaza washindi itakapofanyika jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizo za Wasanii Bora wa Filamu 2012 zilizoandaliwa na Mtandao wa filamucentral zinatarajiwa kutolewa kwa washindi mwezi Februari katika tarehe na ukumbi utakaotajwa na waratibu wake.
Mratibu wa tuzo hizo, Myovela Mfaiswa, aliiambia MICHARAZO kuwa maandalizi kwa ujumla ya hafla hiyo inaendelea vema huku wadau wa filamu wakiendelea kuwapigia kura washiriki wanaochuana katika kinyang'anyiro hicho.
Mfaiswa alisema vipengele vinavyowaniwa katika tuzo hizo zinazofanyika kwa mara ya pili baada ya kufanyika mara ya mwisho mapema mwaka jana kwa wasanii bora wa 2010 ni pamoja na cha Muigizaji Bora wa Kike inayowaniwa na Yvonne Cherry 'Monalisa', Jacklyne Wolper, Wema Sepetu, Jennifer Kyaka 'Odama' na Elizabeth Michael 'Lulu'.
Tuzo nyingine ni ya Mchekeshaji Bora inayowaniwa na wasanii Haji Salum 'Mboto', King Majuto, Sharo Milionea, Kitale na Kinyapi, huku Muigizaji Bora Chipukizi ikiwaniwa na Mariam Ismail 'Mammy', Abdallah Ambua 'Dulla', Slim Omary 'Mdudu Kiu', Jose Mteme 'Baga' na Halima Ali.
Tuzo ya Muigizaji Bora wa Kiume inawaniwa na Jacob Stephen 'JB', Vincent Kigosi 'Ray', Steven Kanumba, Hisani Muya 'Tino' na Single Mtambalike 'Richie', wakati tuzo za Mwandishi Bora wa Mswada inawaniwa na Octavian Natalis, Ali Yakuti, F Kanuti, Elizabeth Chijumba na Kimela Bila.
------
No comments:
Post a Comment