STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, October 16, 2013

Ashanti United yaifumua Prisons, beki Tumba Sued azidi kumfukuzia Tambwe

Na Mahmoud Zubeiry, Chamazi
BAO la dakika ya 90 na ushei la Mwinyi Ally limeipa ushindi wa 2-1 Ashanti United dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni hii Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mchezaji huyo aliyetokea benchi dakika ya 83 kuchukua nafasi ya Fakhi Hakika, alifunga bao baada ya kutokea kizazaa langoni mwa Prisons.
Hadi mapumziko, tayari timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, Prisons wakitangulia kupata bao dakika ya nne kupitia kwa John Matei na beki Tumba Sued akaisawazishia Ashanti dakika ya 21. Hilo lilikuwa bao la nne la Tumba ambalo linamfanya kuwa sambamba na akina Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche na Peter Michael.
Ibrahim Isaka wa Prisons kulia akipambana na Iddi Silas wa Ashanti United leo Chamazi

Prisons inayofundishwa na kiungo wa zamani wa Simba SC, Jumanne Challe ilianza vyema mchezo huo dakika 10 za mwanzo, lakini baada ya hapo, upepo ukabadilika na Ashanti wakauteka mchezo.
Ashanti wangeweza kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa wanaongoza kama si kukosa mabao ya wazi.
Kipindi cha pili, Ashanti inayofundishwa na kiungo wa zamani wa Simba SC, Nico Kiondo iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Prisons na kukosa mabao zaidi ya matatu ya wazi.
Hussein Swedi aliyetokea benchi dakika ya 51 kuchukua nafasi ya Lusako Mwakyusa alikuwa mwiba mkali mbele ya mabeki wa Prisons, lakini alipoteza nafasi mbili za wazi na Paul Maona alipoteza nafasi moja.
Kwa ushindi huo, Ashanti inatimiza pointi nane baada ya kucheza mechi tisa na sasa inasogea hadi nafasi ya 10 kutoka ya 13.
Ashanti United; Daudi Mwasongwe, Hussein Mkongo/Anthony Matangalu dk46, Jaffar Gonga, Tumba Sued, Samir Ruhava, Iddi Silas, Mussa Nampaka, Fakhi Hakika/Mwinyi Allydk83, Paul Maona, Joseph Mahundi na Lusajo Mwakyusa/Hussein Swedi dk51.
Prisons; Beno David, Salum Mashaka, Laurian Mpalile, Lugano Mwangama, Nurdin Issa/Frank William dk82, Omega Seme, John Matei, Freddy Chudu, Peter Michael, Hassan Isaka/Jumanne Elfadhil dk71 na Julius Kwanga/Jeremiah Juma dk47.

No comments:

Post a Comment