LICHA ya kuwatumia nyota wa zamani wa klabu kubwa za soka nchini za Simba, Yanga na Mtibwa, timu ya soka ya Golden Bush Veterani jana uliuaga mwaka 2012 na kuukaribisha kinyonge mwaka 2013 baada ya kutandikwa mabao 4-3 na wapinzani wao wakubwa, Wahenga Fc katika pambano maalum la kirafiki.
Pambano la timu hizo lilifanyika jana jioni kwenye uwanja wa TP Afrika, Sinza Dar es Salaam ambapo Golden Bush, ilijikuta ikipelekwa puta na Wahenga iliyokuwa aikiongozwa na kipa wa zamani wa Yanga na Mtibwa, Mengi Matunda.
Japo Golden Bush, iliyowatumia nyota kama Yahya Issa, Athuman Machuppa, Abuu Ntiro, Waziri Mahadhi, Said Swedi na nduguye Salum Swedi 'Kussi', Nico Nyagawa, Heri Morris, Katina Shija na wengineo iliweza kuongoza kwa mabao 2-1 hadi wakati wa mapumziko, lakini ilishindwa kuepuka kipigio katika mchezo huo.
Golden Bush ilianza kujipatia bao la kuongoza katika dakika ya 18 baada ya Heri Morris kufumua shuti kali lililomshinda kipa wa Wahenga, David 'Seaman' kabla ya Said Swedi kuifungia timu hiyo bao la pili kwa kichwa akiuynganisha krosi pasi ya Nico Nyagawa.
Hata hivyo katika dakika ya 31 Wahenga walipata bao lao la kwanza kupitia kwa mchezaji wao aitwae God aliyeusukumia mpira wavuni kwa shuti karibu na lango lwa Golden Bush.
Kipindi cha pili kilishuhudiwa kwa Golden Bush ikifanya mabadiliko makubwa katika kikosi chao ikiwamo kumtoa Onesmo Waziri 'Ticotico' aliyekuwa akisumbua mbele licha ya kucheza akiwa majeruhi, lakini mabadiliko hayo hayakuwasaidia baada ya Wahenga kutumbukiza wavuni bao la kusawazisha katika dakika ya 65 kupitia Frank 'Super Et'oo'.
Wakati Golden Bush wakitafarakari jinsi walivyofungwa bao hilo, Wahenga walipata bao jingine la tatu lililofungwa kwa njia ya penati na kipa David Seaman katika dakika ya 78 baada ya mmoja wa wachezaji wa timu hiyo kuchezewa rafu ndani ya lango la Golden Bush.
Jahazi la Golden Bush lilizidi kuzama katika dakika ya 82 wakati Wahenga walipojipatia bao lao la nne lililofungwa na beki aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi Shomar aliyewatoroka mabeki wa Golden Bush ambao katika mechi ya jana walionekana kuyumba kusiko kawaida.
Hata hivyo zikiwa zimesalia dakika nne, Golden Bush ilijipatia bao lao tatu la kujifutia machozi, lililofungwa kwa ,mpira wa adhabu ndogo na Salum Swedi 'Kussi' baada ya Machota kuchezewa vibaya na mabeki wa Wahenga nje ya eneo la hatari.
Mara baada ya pambano hilo, Mlezi wa Golden Bush, Onesmo Waziri 'Ticotico' alisema wamekikuibali kipigo cha wapinzani wao, licha ya kwamba alimtupia lawama mwamuzi wa pambano hilo, Ally Mayay kwamba 'aliwauma' na kuahidi kuomba pambano la marudiano na wapinzani wao hao ili kukata mzizi wa fitina.
"TUmekubali kipigo, lakini tutaomba mechi ya marudiano, tunaamini leo tumefungwa kwa sababu mwamuzi alikuwa 'wao', hatuamini kama hawa jamaa wana uwezo wa kuwafunga wakati hivi karibuni tuliwanyuka mabao 4-2 baada ya awali kutokana nao sare ya 1-1," alisema Ticotico.
Hata hivyo baadhi ya watazamaji wa mchezio huo wakieleza kipigo walichopewa Golden Bush kilikuwa halali kutokana na kuzidiwa ujanja na Wahenga, huku wakiwapoingeza walioandaa pambano hilo kwa kuwapa burudani ya kuagia mwaka na kuwashuhudia nyota waliotamba zamani katika klabu mbalimbali nchini ambao walikuwa hawajui wapo wapi kwa sasa baada ya kutoweka kwenye ligi kuu.
No comments:
Post a Comment